In Summary

•Brown alisema kwamba anafahamu mhusika aliye nyuma ya kitendo hicho huku akitishia kulipiza kisasi punde atakapomaliza kukusanya ushahidi.

•Msanii huyo alisema kwamba huwa anatia bidii kubwa katika kazi zake ili kupata mafanikio makubwa ambayo anayo huku akidai kuwa sio lazima atumie njia za udanganyifu ili kufanikiwa.

•Alisema kwamba alishangazwa sana na hatua ya kufutwa kwa ngoma zake ilhali hajakosea ama  kuzozana na yeyote.

Image: INSTAGRAM// OTILE BROWN

Baada ya nyimbo zake tano kufutwa kutoka mtandao wa YouTube, mwanamuziki Jacob Obunga almaarufu kama Otile Brown amejitokeza kuwasuta vikali waliotekeleza kitendo hicho.

Siku ya Jumatano wanamitandao waliamkia habari kwamba nyimbo za Otile Brown k.v.  Dusuma, Chaguo la Moyo, Such Kinda Love, Hi na Aiyana hazikuwepo YouTube tena.

Mwanamuziki huyo ambaye kwa sasa ako katika ziara nchini Afrika Kusini alitumia mtandao wa Instagram kueleza masikitiko yake kufuatia tukio hilo.

Brown alisema kwamba anafahamu mhusika aliye nyuma ya kitendo hicho huku akitishia kulipiza kisasi punde atakapomaliza kukusanya ushahidi.

"Hata sijakasirika, nimesitikishwa na watu wangu. Hawa ni Wakenya ambao wanafanya haya. Ulidhani unafanya kazi, pia sisi tunafanya kazi. Tunakujua tayari lakini nakuahidi tutakapopata ushahidi utajua nguvu zetu pia. Hata wewe hutakula. Tatizo ni kwamba  una roho mbaya, tukiamua kuwa na roho mbaya kama wewe hapa hapatakalika msee. Usione tumenyamaza ukachukulia poa msee" Otile Brown alisema.

Msanii huyo alisema kwamba huwa anatia bidii kubwa katika kazi zake ili kupata mafanikio makubwa ambayo anayo huku akidai kuwa sio lazima atumie njia za udanganyifu ili kufanikiwa.

"Mimi ni mkweli. Sio lazima nidanganye ili nifanikiwe. Sio lazima nitumie njia rahisi kwa mambo ambayo hayana maana kwangu. Kama ni rahisi sitaki. Najivunia wakati nang'ang'ana na kupata matokeo makubwa. Wakati naipambania na kupata ndio furaha yangu. Ni tamu zaidi. Nakumbatia mashida zangu kama mwanaume" Alisema Otile Brown.

Otile alidai kwamba hana ugomvi ya yeyote na huwa hadhalilishi mtu yeyote hata wanaojifanya wema ilhali wana nia mbaya.

Alisema kwamba alishangazwa sana na hatua ya kufutwa kwa ngoma zake ilhali hajakosea ama  kuzozana na yeyote.

"Unaangazia mambo yasiyofaa. Nyimbo zote kubwa unazichukua. Sababu gani?Nimekufanyia  nini mimi? Wengine wenu ata huwa hatupatani. Mi nafanya kazi zangu. Mimi na wewe hatujawahi patana, unachukua vitu vyangu kwa sababu gani? Sijawahi kukosea hata siku moja. Mimi naheshimu kila binadamu. Mimi ni mtu tofauti. Napenda kila mtu, naheshimu kila binadamu, sijawahi dharau mtu hata siku moja. Huwa nakutana nao hata wakiweka tabasamu bandia. Watu walewale ambao unapatana nao wakitabasamu wanajifanya washikaji. Tunawajua ndugu. Naweza jua mnafiki ata akijifanya" Otile alisema.

Brown sio mwanamuziki pekee ambaye nyimbo zake zimefutwa kwenye mtandao wa YouTube. Baadhi ya nyimbo za  Nadia Mukami, Nviri The Storyteller na Bensoul pia zimefutwa.

View Comments