In Summary

•Kulingana na Juliani, familia ya DJ Evolve ilifanya uamuzi wa kuondoa kesi hiyo kwa kuwa walielewa fika kwamba ni ghali sana kupata haki hapa nchini.

DJ Evolve na Juliani
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani ametetea hatua ya mcheza santuri Felix Orinda (DJ Evolve) kuondoa kesi ya jaribio ya mauaji dhidi ya mbunge wa Embakasi Babu Owino.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Juliani amesema hali ya kutofanikiwa kifedha sio ya kunyooshewa kidole katika suala hilo.

Kulingana na Juliani, familia ya DJ Evolve ilifanya uamuzi wa kuondoa kesi hiyo kwa kuwa walielewa fika kwamba ni ghali sana kupata haki hapa nchini.

"Hatuwezi kulaumu umaskini kwa hadithi hiyo ya DJ Evolve. Yeye na familia wanaelewa jambo moja, haki ni ghali na maskini hawawezi kumudu" Juliani alisema.

Siku ya Jumanne mahakama ilikubali wasilisho la Elvolve la kuondolea mbunge huyo wa muhula wa kwanza kesi ya jaribio la mauaji.

Babu amekuwa akijaribu kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama. Wakili wa familia ya DJ Evolve aliambia mahakama kuwa wako katika hatua za mwisho za mazungumzo. 

Upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa mazungumzo yamekuwa yakiendelea kati ya pande hizo mbili.

Mahakama ilisikia kwamba upande wa mashtaka ulifanya mikutano miwili kati ya Babu na Evolve pamoja na mawakili.

Hata hivyo, Babu atashtakiwa katika shtaka la pili la kujiendesha kwa fujo huku akiwa amebeba bunduki

Mbunge huyo alishtakiwa kwa kujaribu kumuua Evolve ambaye alimpiga risasi katika kilabu kimoja jijini Nairobi mnamo Januari 2020.

View Comments