In Summary

•Raburu alitangaza kifo cha babu yake, Ker Willis Opiyo Otondi siku ya Ijumaa asubuhi na kusema kwamba ni pigo kubwa kwake na inauma.

•Raburu alifichua kwamba ameridhi jina la marehemu na kufuatia hilo akaahidi kuendelea kuliheshimisha siku zote.

Babu ya Willis Raburu, Willis Opiyo Otondi ameaga dunia
Image: INSTAGRAM// WILLIS RABURU

Mtangazaji na mburudishaji maarufu Willis Raburu yuko katika hali ya maombolezo.

Raburu alitangaza kifo cha babu yake, Ker Willis Opiyo Otondi siku ya Ijumaa asubuhi na kusema kwamba ni pigo kubwa kwake na inauma.

"Inawezekanaje lakini eti jana tu tulikuwa tunazungumza na leo ..."  aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha kadhaa za kumbukumbu za marehemu ambaye alionekana katika miaka ya uzeeni.

Willis alimkumbuka Bw Opiyo kama mtu mwenye kuzungumza mawazo  yake, mkali na mwenye furaha na tabasamu nzuri.

"Ulisimama kidete. Ulitujali sote na ulitaka kuhusika katika maisha yetu," Willis alisema kuhusu marehemu.

Mtangazaji huyo alifichua kuwa babu yake alikuwa mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kijaluo na kusema matendo yake wakati akitumikia nafasi hiyo yatakumbukwa daima.

Pia alifichua kwamba ameridhi jina la marehemu na kufuatia hilo akaahidi kuendelea kuliheshimisha siku zote.

"Ninaishi kuheshimu urithi na kumbukumbu yako kwa kutangaza jina lako! Nimebarikiwa na kuheshimiwa kuendelea na jina Willis Edwin Opiyo Otondi,"

Willis alimtakia babu yake mapumziko ya amani na kusema  kwamba atamkosa sana.

View Comments