In Summary

•Githae aliweka wazi kuwa hafahamu kuhusu kundi lolote lililoundwa kumchangia pesa DJ Fatxo kama ambavyo imekuwa ikidaiwa hivi majuzi.

•Githae aliwataka Wakenya kuwa watulivu huku wakisubiri wapelelezi wanaoshughulikia suala hilo kukamilisha kazi yao.

Mwimbaji Ben Githae

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili na za kisiasa Ben Githae ametupilia mbali madai kwamba wasanii wameungana kumsaidia DJ Fatxo kwa gharama za kisheria baada ya kuhusishwa na kifo cha Geoffrey Mwathi (Jeff).

Kwenye mahojiano na Nairobi News, mwanamuziki huyo wa nyimbo za Kikuyu aliweka wazi kuwa hafahamu kuhusu kundi lolote lililoundwa kumchangia pesa DJ Fatxo kama ambavyo imekuwa ikidaiwa hivi majuzi.

"Hatuko katika kundi lolote. Hizo ni propaganda tu, lakini tunaomba haki, na hiyo iambatane na ukweli,” alisema.

Githae aliwataka Wakenya kuwa watulivu huku wakisubiri wapelelezi wanaoshughulikia suala hilo kukamilisha kazi yao.

Jeff alifariki mnamo Februari 22 na ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi iliashiria kuwa alijitoa uhai kwa kuruka  kupitia dirisha la nyumba ya mwimbaji maarufu wa Mugithi, Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo.

Walioandikisha taarifa katika kituo cha polisi walieleza kuwa kijana huyo wa miaka 23 aliwahi kuwa na mawazo ya kujitoa uhai miaka ya nyuma. Walidai kuwa aliruka kutoka orofa ya kumi ya jengo hilo na kukatisha maisha yake papo hapo bila ufahamu wa watu ambao alikuwa nao ndani ya nyumba ya DJ Fatxo.

Hali kuhusu kifo cha Jeff na jinsi kilivyoshughulikiwa hata hivyo imetiliwa shaka sana na Wakenya wenye hasira haswa kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakiwaagiza wapelelezi kufanya uchunguzi wa kina.

Tetesi\ ziliibuka kuwa wasanii wenzake DJ Fatxo wameungana ila kumsaidia katika kesi hiyo ambayo amehusishwa nayo.

Akizungumza na Nairobi News, Githae aliweka wazi kuwa wasanii huungana na kusaidiana wakati mmoja wao anapokumbwa na tatizo la kinyumbani.

Aidha, alilalamika kuwa mashabiki wanawahuku wasanii vikali na wakati mwingine hata kusahau kuwa wao ni binadamu na wana hisia pia.

“Wanakuinua, lakini wakiona umetengeneza na kupata fedha kupitia wao, wanaanza kukupiga. Wakisikia kuwa umewatelekeza watoto wako, wanakukanyaga. Huwezi kuelewa mashabiki wetu. Wanataka tufanye nini?” Alihoji.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inaendelea kufanya uchunguzi wa kina katika kesi ya kifo cha kijana huyo wa miaka 23.

View Comments