In Summary

•King Chelsea ambaye ni maarufu kwa kuvaa nguo za kiume na za kike alifichua kuwa alichora tattoo ya Fantana kwenye goti lake kutokana na mapenzi yake kwake.

•'Wow, hii ni tamu sana. Nakupenda zaidi," Fantana alisema.

Fantana amejawa bashasaha baada ya jamaa kuchorwa tatto yake
Image: HISANI

Mwanamuziki mashuhuri wa dancehall kutoka Ghana, Francine Kouffie almaarufu Fantana ameachwa na mshangao mkubwa baada ya mmoja wa mashabiki wake kuchora jina lake kwenye ngozi yake.

Jumatano, mwanamtandao mwanaume kwa jina King Chelsea ambaye ni maarufu kwa kuvaa nguo za kiume na za kike alifichua kuwa alichora tattoo ya Fantana kwenye goti lake kutokana na mapenzi yake kwake.

“Nilipitia uchungu kwa ajili tu ya huyu binti ninampenda sana na natamani nimuone,” King Charles alisema huku akionyesha tattoo hiyo.

Alisema hamu yake kubwa ni kukutana na msanii huyo mwenye umri wa miaka 25 na hivyo akawaomba watu wamsaidie kumfikia.

"Jinsi ninavyompenda msichana huyu ni Mungu pekee anajua. Jameni naomba mnisaidie nimuone," aliomba.

Aliongeza, "Mpenzi wangu Fantana naomba uniruhusu nikuone kwa sababu nilipitia maumivu haya kwa sababu yako."

Kwa bahati nzuri, ombi la King Chelsea lilimfikia mwimbaji huyo ambaye alishiriki  video zake kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Fantana alisema kuwa kitendo cha jamaa huyo ni cha kupendeza sana na akadhihirisha upendo wake mkubwa kwake.

'Wow, hii ni tamu sana. Nakupenda zaidi," Fantana alisema.

Hata hivyo, hakufichua kama ana mpango wa kukutana na King Chelsea kulingana na ombi lake au jinsi anavyopanga kumtuza.

Wiki za hivi majuzi, Fantana amekuwa akitajwa kuwa kwenye mahusiano wa kimapenzi na staa wa bongo Diamond Platnumz.

Uvumi huo uliibuka baada ya kupeperushwa kwa kipindi cha pili cha filamu ya Young, Famous and African kwenye Netflix.

Katika moja ya matukio kwenye filamu hiyo, Diamond alionekana akishiriki muda mzuri na Fanatana na hata kubusiana kimahaba 

“Nilijiona mimi ndiye bora kwa kubusu, hadi nilipombusu Fantana,” Diamond alisema kuhusu tukio hilo la kubusiana.

Alibainisha kuwa busu la Fantana lilikuwa zaidi ya busu.

"Hakuwa ananibusu, alikuwa akinila!" alisema.

Diamond aliweka wazi kuwa busu la malkia huyo wa Ghana lilikuwa bora zaidi kuwahi kupokea katika miaka yote 32 ya kuwepo kwake.

Fantana ni mwimbaji na mwanamitindo wa Ghana ambaye ni mmoja wa wahusika wa kipindi cha Young, Famous and African. Hata hivyo, hana historia ya mahusiano na Diamond mbali na kuwa washiriki wa YFA2.

View Comments