In Summary

•Wakati akichukua hatua hiyo kubwa, Bahati alibainisha kuwa amekamilisha hatua zote muhimu kuelekea ndoa na sasa yuko tayari kuifanya rasmi.

•Kwenye ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo alitangaza tarehe 12 Desemba kuwa siku ya harusi yao.

Image: YOUTUBE// DIANA MARUA

Mwimbaji mashuhuri wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati alimchumbia rasmi mpenzi wake wa muda mrefu na mzazi mwenzake Diana Marua.

Wawili hao walirekodi kipindi hicho kizuri katika video iliyopeperushwa kwenye chaneli ya YouTube ya Diana Marua siku ya Jumatatu.

Wakati akichukua hatua hiyo kubwa, Bahati alibainisha kuwa amekamilisha hatua zote muhimu kuelekea ndoa na sasa yuko tayari kuifanya rasmi.

"Umenipatia moyo wako. Kusema kweli kutoka ndani ya moyo wangu, siichukulii virahisi. Kitu kimoja ambacho ninataka sana kufanya mwaka huu, nataka tu kuhakikisha nimefanya sawa, najua nimeenda kwa familia yako kwa utambulisho lakini mwaka huu nataka tufanye harusi ya kweli na nataka kukuoa," Bahati alimwambia mchumba wake.

Aliongeza, "Nataka kuhakikisha kwamba nimekuoa kiroho rasmi. Mungu anajua moyo. Nataka kuifanya kwa utamaduni. Kwa heshima ya wazazi wako, baba yako, nakuahidi kwamba mwaka huu nitakufanyia harusi kubwa na bora zaidi ambayo macho yako yamewahi kuona. Hiyo ndiyo ahadi yangu."

Pindi tu baada ya kusema maneno hayo matamu kwa Diana ambaye wakati huo tayari alikuwa amezidiwa na hisia kali, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alitoa pete ambayo alikuwa ameibeba kwenye kasha dogo na kisha kumuuliza mama huyo wa watoto wake watatu iwapo ataolewa naye.

"Nataka kuchukua fursa hii kukuonyesha kwamba namaanisha hilo na nakuthamini. Ndiyo maana nataka kufanya upya viapo vyetu. Nataka kukuuliza kwa mara nyingine, "Je, utaolewa nami?" alimuuliza.

Huku akibubujikwa na machozi, Diana Marua alijibu, "Ndiyo. Nakupenda sana na nasema ndiyo mara milioni. Na asante."

Mama huyo wa watoto watatu aliendelea kububujikwa na machozi ya furaha kabla ya kueleza jinsi anavyotazamia siku hiyo kubwa katika maisha yao ambapo hatimaye watarasimisha ndoa yao.

"Najua tumekuwa tukipanga. Tumeongea kuhusu hili lakini sasa ni kweli kabisa. Itafanyika. Siwezi kusubiri kufunga pingu za maisha na kusema ndiyo mbele ya kanisa, dunia yote na mbingu. Naahidi kwamba siku zote nitajisalimisha kwako. Nakupenda sana kila siku," Diana alimwambia mpenziwe.

Kando na pete, Bahati pia alimpa mchumba wake hereni kama ishara ya uchumba.

"Ninataka kuzeeka na wewe, kusafiri ulimwengu na wewe, kusafiri ulimwengu na watoto wetu pamoja na wewe. Nitasema ndiyo kila siku. Mungu atulinde kila siku," Diana alimhakikishia mwanamuziki huyo.

Baadaye, kwenye ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo alitangaza tarehe 12 Desemba kuwa siku ya harusi yao.

"Alisema ndiyo.  Na natangaza rasmi kwamba Desemba 12 ni siku ya harusi yetu," Bahati alisema.

View Comments