In Summary

•DJ Fatxo ametoa shukrani kwa mashabiki waliosimama naye kwa muda wa takriban miezi mitatu aliokuwa akikabiliwa na madai ya mauaji na ushoga.

•Fatxo alibainisha kuwa licha ya matusi mengi makali, baadhi ya mashabiki wake wa dhati hawakuyumbishwa na waliendelea kusimama naye.

Image: FACEBOOK// DJ FATXO

Mwimbaji wa Mugithi Lawrence Njuguna Wagura almaarufu DJ Fatxo ametoa shukrani kwa mashabiki waliosimama naye kwa muda wa takriban miezi mitatu aliokuwa akikabiliwa na madai ya mauaji na ushoga.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili jioni, DJ Fatxo ambaye mwezi uliopita aliondolewa mashtaka ya mauaji ya rafiki yake Jeff Mwathi alibainisha kuwa baadhi ya mashabiki wake waliitwa majina ya kejeli walipojaribu kumtetea.

"Kando na Thendekia & Gatina FC, ni jina gani ulilofanya ulipojaribu kunitetea?" DJ Fatxo alihoji kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Alibainisha kuwa licha ya matusi mengi makali, baadhi ya mashabiki wake wa dhati hawakuyumbishwa na waliendelea kusimama naye.

Kufuatia sapoti hiyo, mwanamuziki huyo aliwashukuru mashabiki hao na kuwahakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwao.

“Nawaombea ninyi nyote mliosimama na ukweli. Nawapenda. Wale wa matusi pia nawashukuru. Ni kwa sababu yako nimegundua upande wangu wenye nguvu ambao sikuwa nao,” mwimbaji huyo wa Mugithi aliandika.

Aliambatanisha taarifa hiyo na picha ikimuonyesha akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake, ishara kuwa ameweza kukabiliana na masaibu yaliyomkumba.

Mwezi jana, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma aliwaondolea DJ Fatxo na wenzake mashtaka ya mauaji ya Jeff Mwathi na kueleza ni kwa nini hakuna hata mmoja aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha kijana huyo wa miaka 23.

Katika barua kwa Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) iliyotiwa saini na mkurugenzi msaidizi wa mashtaka ya umma Gikui Gichuhi, DPP alitaja ushahidi uliowaondolea washukiwa hao mashtaka.

Huku akijibu madai ya kuwa shoga mwezi uliopita, Fatxo alijitenga mbali na kundi la wapenzi wa jinsi moja almaarufu LGBTQ.

Katika mahojiano na Mpasho, alisema madai  ya ushoga ni uvumi tu ulioanzishwa na kuenezwa na maadui zake ambao hakufichuliwa.

Alibainisha kwamba hata hajawahi kupatwa na wazo la kuwa mpenzi wa jinsia moja

"Sijawahi kuwa, sitawahi kuwa na mimi si wa LGBTQ," Fatxo alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za Kikuyu mwenye umri wa miaka 27 aliweka wazi kuwa anawapenda sana wanawake na wanampenda pia.

"Kuhusu kuwa mashoga, wanawake wananipenda na mimi nawapenda. Mimi sio shoga na siwezi," alisema.

View Comments