In Summary

•Wanjeri alifichua kuwa tayari mama yake alikuwa ameenda kuwa naye nyumbani kwake, jambo ambalo lilimridhisha sana moyoni.

•Mamake Wanjeri hata hivyo alimkosoa bintiye kwa kumdanganya hapo awali na akapinga madai kuwa alimruka.

Leting Kenya, Mamake Nyce Wanjeri, Nyce Wanjeri
Image: FACEBOOK// NYCE WANJERI

Siku ya Jumatano, Muigizaji Nyce Wanjeri almaarufu Auntie Boss kutokana na kipindi cha Televisheni cha ‘Auntie Boss’ kwenye NTV alidokeza kwamba alikuwa karibu kumkaribisha mtoto wake wa kwanza duniani.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, Wanjeri alifichua kuwa tayari mama yake alikuwa ameenda kuwa naye nyumbani kwake, jambo ambalo lilimridhisha sana moyoni.

Pia alibainisha kuwa kuwasili kwa mzazi huyo wake ilikuwa ishara kwamba siku yake ya kujifungua imewadia.

“Moyo wangu umejaa. Mama yuko nyumbani. Ukiona mum amekuja unajua karibu Mungu anene. Asante Mungu,” Wanjeri aliandika chini ya picha yake, mamake na mumewe Leting Kenya ambayo aliichapisha kwenye Facebook.

Katika picha hiyo, watatu hao walionekana kusisimka sana na huku tumbo la Wanjeri likionekana kuwa kubwa zaidi kuliko hapo awali.

Hata hivyo baadaye siku ya Alhamisi, muigizaji huyo mcheshi alichapisha video ya mama yake na mumewe wakimpeleka hospitali ambapo walishauriwa kurudi nyumbani, jambo ambalo lilionekana kumsononesha.

"Sema kurudishwa nyumbani na vile nakaa ka python imemeza mbuzi," Wanjeri alilalamika.

Katika video hiyo, alibainisha kuwa alikuwa tayari sana kujifungua siku ya Alhamisi na kwa kejeli akamlalamikia mamake kwa kutofanya ambavyo walikuwa wamekubaliana.

“Situmerudishwa nyumbani unaniuliza (Leting) ni nini na nilikuwa tayari leo... Mum unaweza niruka hivyo na daktari na vile tulikuwa tumebonga,” alisema.

Mamake Wanjeri hata hivyo alimkosoa bintiye kwa kumdanganya hapo awali na akapinga madai kuwa alimruka.

“Ata nyinyi mlinidanganya. Mliniambia siku ya kuandikisha tarehe moja,” mamake Wanjeri alisema.

Wanjeri hata hivyo alidokeza kuwa yeye na mume walidhani siku yake ya kujifungua ilikuwa imefika.

Mwishoni mwa video hiyo, Bw Leting alisikika akimwambia mkewe kwa utani kwamba itabidi wasubiri mwezi mwingine mmoja.

View Comments