In Summary

•Tembu Daniel almaarufu Towncryer amefunguka kuhusu changamoto alizokabiliana nazo katika jaribio hilo lake. 

•Alifichua kwamba jaribio hilo hatari pia lilimuacha akikabiliana na maumivu ya kichwa, macho yenye uvimbe, na uso uliofura.

Image: INSTAGRAM// TOWNCRYER

Mburudishaji wa Nigeria ambaye alijaribu kuvunja Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa saa ndefu zaidi alizotumia mtu binafsi kulia, Tembu Daniel almaarufu Towncryer amefunguka kuhusu changamoto alizokabiliana nazo katika jaribio hilo lake. 

Awali, Daniel alilenga kulia kwa saa mia moja na kuvunja Rekodi ya Dunia lakini aliweza kulia kwa takriban saa sita tu.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na BBC News, jamaa huyo raia wa Cameroon anayeishi Nigeria alifichua kwamba alipofuka kwa muda kwa takriban dakika 45 alipokuwa kwenye mbio za kuweka rekodi mpya ya dunia.

Danny alisema kuwa kutokana na hilo alilazimika kupunguza kilio chake.

"Ilinibidi kupanga upya mikakati na kupunguza kilio changu," alisema.

Alifichua kwamba jaribio hilo hatari pia lilimuacha akikabiliana na maumivu ya kichwa, macho yenye uvimbe, na uso uliofura.

Daniel alianza safari ya kulia kwa saa mia moja bila kukoma mapema wiki jana akiwa na matumaini ya kuweka rekodi mpya ya dunia.

Kwa idhini ya Rekodi za Dunia za Guinness, kama ilivyothibitishwa katika bango ambalo alionyesha, alidhamiria kufikia mafanikio hayo ya kushangaza.

“Nitaenda kuvunja rekodi ya dunia ya Guiness kwa muda mrefu zaidi nikilia. Nahitaji usaidizi wenu,” Daniel alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram wikendi ya wiki jana.

Baadaye alishiriki klipu ya video iliyoonyesha akianza safari yake ya saa 100 za kilio ambapo alionekana akiwa ameketi kwenye kiti huku saa kubwa iliyokuwa ikisonga ikiwa kando yake.

Katika taarifa nyingine, mtayarishaji wa maudhui huyo ambaye kwa sasa anaishi Lagos, Nigeria alionyesha kuwa tayari alikuwa amelia kwa masaa mawili. Pia aliwataarifu wafuasi wa mtandaoni baada ya kulia kwa zaidi ya saa tano.

Video zilizomuonyesha akilia huku saa iliyokuwa kando yake ikiendelea kusonga zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia mseto baina ya wanamitandao. Baadhi walimtia moyo huku wengine wakimkejeli kwa jaribio hilo.

View Comments