In Summary

• Nyamu alifichua kuwa Samidoh alihusika sana na kesi ya kutatua kifo cha mpwa wake ingawa hakufanya hivyo machoni pa umma.

•Nyamu aliwakosoa Wakenya kwa kumuangazia sana DJ Fatxo ilhali ushahidi uliokuwepo ulidokeza kuwa sio yeye aliyemuua.

Karen Nyamu na marehemu Jeff Mwathi
Image: HISANI

Mwanasiasa na wakili maarufu Karen Nyamu amebainisha kuwa Wakenya walimhukumu vibaya mpenzi wake Samidoh kuhusiana na kesi ya kifo cha mpwa wake Jeff Mwathi takriban miezi mitano iliyopita.

Jeff, ambaye ni mpwa wa mwimbaji huyo wa mugithi alifariki kwa njia isiyoeleweka mnamo Februari 22 mwaka huu alipokuwa nyumbani kwa DJ Fatxo na wanamitandao wa Kenya walimsukuma sana Samidoh kutoa maoni yake kuhusu kisa hicho na kuhusika katika kesi ikizingatiwa kuwa licha ya mwathiriwa kuwa jamaa yake, mmoja wa washukiwa waliotajwa ni mwimbaji mwenzake wa mugithi.

Katika mahojiano na Ala C katika kipindi cha Reke Ciume na Ene, Nyamu alifichua kuwa mzazi huyo mwenzake alihusika sana na kesi ya kutatua kifo cha mpwa wake ingawa hakufanya hivyo machoni pa umma.

“Bila shaka watu walimhukumu (Samidoh) vibaya. Hakuna chochote hakufanya. Hata mawakili waliokuwa wakishughuliki kesi hiyo ni mawakili wake binafsi. Hao ndio wanaofanya kazi zake na ni wale wale ambao walikuwa wakishinda Kiambu siku nzima na mamake Jeff," Karen Nyamu alisema.

Seneta huyo ambaye pia ni wakili pia aliwakosoa Wakenya kwa kumuangazia sana DJ Fatxo na kumchukua kama mshukiwa pekee ilhali ushahidi uliokuwepo ulidokeza kwamba haiwezekani kuwa yeye ndiye aliyemuua kijana huyo wa miaka 23.

"Hata kama ilitokea nyumbani kwake, ingawa anaweza kujua ni nani aliyefanya hivyo, sio yeye. Inaonekana kwamba wakati Jeff alikufa, Fatxo alikuwa nje ya nyumba. Uchunguzi unaonyesha hivyo,” alisema.

Nyamu alisema umma ulimwangazia sana DJ Fatxo na kukosa kuelekeza macho yao kwa watu wengine waliokuwa ndani ya nyumba yake wakati mpwa wa Samidoh alipokumbana na kifo chake.

Alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba mmoja wa wale waliokuwa ndani ya nyumba hiyo anaweza kuwa na hatia ya kifo hicho cha kutatanisha ambacho bado hakijatatuliwa hadi sasa.

“Sitaki kumsafisha Fatxo lakini pengine akilini mwake alijua hakufanya kitendo hicho lakini labda alijua. Hayo ni mawazo yangu tu, sisemi ukweli. Ninasema kile ninachofikiria kawaida," alisema.

Seneta huyo wa kuteuliwa alisema mamake Jeff ni rafiki wa karibu sana naye na akafichua kwamba huwa anazungumza naye mara kwa mara na kumtia moyo anapoendelea kukabiliana na kifo cha mwanawe.

View Comments