In Summary

•Kimani amewaomba watu wema kumtumia kiasi chochote cha pesa kupitia nambari yake mpya ya simu ambayo ametoa.

•Kimani pia aliahidi kuwafahamisha Wakenya kuhusu jinsi pesa watakazochangia kwa ajili yake zitatumika.

Kimani Mbugua Aliyekuwa mtangazaji wa Citizen TV Kimani Mbugua
Image: Instagram

Aliyekuwa mtangazaji wa Citizen TV Daniel, Kimani Mbugua ametoa taarifa zaidi kuhusu ombi lake la usaidizi kwa Wakenya.

Kimani ambaye hivi majuzi alifunguka kuhusu matatizo yaliyomkumba na kufichua kuwa kwa sasa hana makazi amewaomba watu wema kumtumia kiasi chochote cha pesa kupitia nambari yake mpya ya simu ambayo ametoa.

Katika taarifa yake ya Jumatatu asubuhi, alifichua kuwa anahitaji takriban 200,000 ili kuanzisha kampuni yake ambayo anatumai itamtoa kwenye matatizo.

“Habari zenu, nashukuru sana kwa msaada mkubwa kutoka kwenu wote, asanteni sana. Sikuwa hata na simu wala namba ya mpesa nilipoweka video hiyo, hii hapa nambari yangu mpya (0741954681),” Kimani alisema kupitia Instagram.

Aliongeza, “Namba yangu nyingine 0718.. ilipitishwa kwa mtumiaji mwingine, hii hapa namba yangu mpya, tafadhali tuma chochote unachoweza ata 1 bob ni sawa.. Nahitaji kuongeza mtaji wa kampuni yangu (200k).”

Kimani pia aliahidi kuwafahamisha Wakenya kuhusu jinsi pesa watakazochangia kwa ajili yake zitatumika.

Wiki iliyopita, mwanahabari huyo alichapisha video kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo aliomba msaada wa kusimama tena baada ya kuondoka hospitalini takriban wiki moja kabla.

“Nilitoka hospitalini wiki iliyopita na nahisi akili yangu imerejea katika hali ya kawaida na sitaki kurudi nilipokuwa zamani,” alisema.

Mbugua alibainisha kuwa kwa sasa hana makao kwani watu waliomkaribisha kwao hapo awali walimwambia atafute mahali pengine.

"Nilikuja kutafuta mtu mwingine ambaye angeweza kunikaribisha lakini sikumpata. Nahitaji msaada wenu," alisema.

Mbugua alisema hajatumia dawa za kulevya kwa muda wa miezi miwili iliyopita na hatataka kurejea hapo tena. Alisema alikuwa akitumia vibaya bangi na sigara. Alisema hatimaye yuko katika hatua ya kupona hata kama hana mahali pa kukaa.

Alisema alipoteza vitu mingi sana ikiwa ni pamoja na marafiki katika safari yake ya kupona.

“Niko katika hali ambayo watu wengi hawako tayari kusaidia, wanasema wamechoka,” alisema.

Alibainisha kuwa hata aliazima simu ambayo aliitumia kuchukua video hiyo akiomba msaada na kuiweka kwenye mitandao ya kijamii.

“Ukitaka kunisaidia, barua pepe yangu ni danielkimani2027@gmail.com,” alisema.

Kimani alisema ndani ya wiki moja ambayo ametoka hospitalini, tayari amekuja na mpango wa biashara na pendekezo lake la kwanza kwa mteja mwenye muundo wa kampuni. Alisema kwa sasa anatafuta mfanyibiashara makini ambaye atawekeza pesa za kusaidia wazo lake kuanza.

Alisema hataki kuteseka kimya kimya na hivyo kuamua kutafuta usaidizi kutoka kwa Wakenya.

"Niligundua kuwa naweza kuteseka kimya kimya na nisiseme na kushuka moyo tena na kurudi kwenye dawa za kulevya. Sitaki kurejea kwenye dawa za kulevya," alisema.

View Comments