In Summary

•Kajala aliweka video ya mkono wake wa kushoto ukiwa na pete na akaeleza kuwa amechukuliwa na ameridhika.

• Kajala alishare ujumbe akidokeza kwamba amepata mwanamume ambaye anamtaka na kubainisha kwamba ameridhika. 

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Kuna uwezekano mkubwa kuwa muigizaji mkongwe wa Tanzania Frida Kajala Masanja hayupo tena sokoni.

Posti ya hivi punde ya mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize kwenye Instagram inadokeza kuwa amevishwa pete ya uchumba na mpenzi wake.

Kajala aliweka video ya mkono wake wa kushoto ukiwa na pete kwenye kidole cha pete na katika sehemu ya maelezo akaeleza kuwa amechukuliwa na ameridhika.

"Mkono wangu unajisikia mzito leo... Nashangaa kwa nini.. Nimechukuliwa na kufurahi," Kajala aliandika na kuambatanisha ujumbe huo kwa emoji ya moyo kuashiria mapenzi.

Wiki iliyopita, mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba tayari anachumbiana na mwanamume mwingine na kwamba wako kwenye uhusiano wenye furaha.

Jumatano wiki jana, Kajala alishare ujumbe akidokeza kwamba amepata mwanamume ambaye anamtaka na kubainisha kwamba ameridhika. 

“Nimepata mwanaume ninayemtaka, nimefurahi,” ujumbe huo ulioshirikishwa na Kajala kwenye Instastori ulisomeka.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 hata hivyo hakushiriki maelezo zaidi kuhusu uhusiano wake mpya au mwanaume ambaye amechukua nafasi ya Harmonize. 

Haya yanajiri takriban miezi kumi baada ya uhusiano wake na bosi wa Konde Music Worldwide kufika kikomo baada ya kuchumbiana miezi kadhaa. Mastaa hao walikuwa wamerudiana mwezi Mei mwaka uliopita baada ya kutengana mwaka mmoja kabla. Harmonize alifanya juhudi nyingi kumuomba msamaha Kajala na kumtongoza katika juhudi za kumshawishi akubali kufufua uhusiano wao uliovunjika.

Wakati akitangaza kuachana na mwanamuziki huyo mwezi Desemba, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema wakat huo.

Wakati wa mahojiano na kituo cha redio cha hapa nchini mapema mwaka huu, Kajala alidokeza kuwa alimtema Harmonize kwa sababu ya mazoea.

"Sijui niseme nini. Labda mazoea. Mtu akishakuzoea sana anakuchukulia poa," alisema.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alidokeza kwamba Harmonize bado hakuwa tayari wakati alipoamua kutulia naye kwenye mahusiano na kuwa huenda alihitaji nafasi ya kufanya mambo yake binafsi.

"Yaani mimi hata simlaumu, kwa sababu yeye ni kijana mdogo. Labda alihitaji nafasi, tulikuwa tuko karibu sana.

Yeye mara ya kwanza nahisi labda aliona kama mzaha akisema nataka huyu mtu, nataka niwe naye 24/7.  Mnaamka wote mnaenda gym, mnafanya hiki na kile. Labda alikuwa anahitaji nafasi yake afanye vitu vyake," alisema.

Kajala alibainisha kwamba alikubali kurudaina na bosi huyo wa Konde Music Worldwide kwa kuwa bado alikuwa anampenda.

View Comments