In Summary

•Kumekuwa na tetesi nyingi zinazodai kuwa afya ya muigizaji huyo imeendelea kuzorota na kuwa amekatwa miguu yake yote miwili.

•Familia imebainisha kuwa haijampeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi kwani imetangazwa kuwa "hafai kusafirishwa kwa ndege."

Bw John Okafor hospitalini.
Image: HISANI

Familia ya muigizaji mkongwe wa Nigeria Bw John Okafor almaarufu Mr Ibu imejitokeza kufafanua kuhusu uvumi mbalimbali kuhusu afya ya msanii huyo ambao umekuwa ukienezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Katika siku chache zilizopita, kumekuwa na tetesi nyingi zinazodai kuwa afya ya muigizaji huyo imeendelea kuzorota na imedaiwa kuwa amekatwa miguu yake yote miwili.

Jumapili hata hivyo, familia ya Bw Okafor ilifutilia mbali uvumi huo ikiweka wazi kuwa ni mguu mmoja tu wa muigizaji huyo ambao ulikatwa mwezi uliopita.

"Tunapenda kutoa shukurani zetu za dhati kwa Wanigeria na umma kwa ujumla kwa mchango wenu mkubwa, wa kimwili, kiroho na zaidi ya yote kifedha kwa kumfanya baba yetu Bw John Okafor (Bw Ibu) asimame," familia ya Bw Okafor ilisema katika taarifa.

Katika taarifa hiyo iliyoshirikiwa kwenye akaunti rasmi ya Instagram ya muigizaji huyo, familia hiyo ilithibitisha kwamba hata hivyo kulikuwa na kukatwa kwa mara ya pili kwenye mguu huo huo ambao ulipashwa kisu mwezi uliopita.

"Tunataka kurekebisha madai potofu yanayoenea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hali ya sasa ya afya ya baba yetu. Kwanza tungependa kusema kwamba baba yetu hakukatwa miguu yote miwili bali mmoja tu. Kukatwa kwa mara ya kwanza hakukusahihisha kabisa hali yake ya kiafya kwa hivyo daktari alilazimika kwenda mbele kumkata mguu huo huo ili kuhakikisha hatumpotezi,” iliongeza taarifa hiyo.

Ikifafanua kuhusu ugonjwa wa muigizaji huyo, familia hiyo ilisema, "Chanzo cha ugonjwa wa baba sio ugonjwa wa kisukari lakini alikuwa na damu iliyoganda mara kwa mara kwenye mguu wake (mishipa yenye ugonjwa) na changamoto zingine za kiafya zilizohatarisha maisha yake, kwa hivyo hitaji la kukatwa."

Familia ilibainisha kuwa haijampeleka muigizaji huyo mkongwe nje ya nchi kwa matibabu zaidi kwani daktari amemtangaza kuwa "hafai kusafirishwa kwa ndege."

"Baba kwa sasa amelazwa katika mojawapo ya hospitali kubwa na bora zaidi tulizo nazo nchini Nigeria kufikia leo na hospitali imempatia kundi la wataalamu shupavu," walisema.

Familia iliwahakikishia mashabiki, marafiki na mastaa wenza wa muigizaji huyo kwamba anaendelea kupata nafuu lakini hata hivyo wakawaomba waendelee kutoa sapoti na maombi hadi atakapopona kabisa.

View Comments