In Summary

•Mwana Mtule amekuwa mtu huru baada ya kuachiliwa kutoka KNH ambako inadaiwa alikuwa akizuiliwa kwa wiki chache zilizopita.

•Ili kuthibitisha kuwa sasa yuko sawa, aliambatanisha kauli yake na video yake akifanya sanaa yake maarufu ya kumuiga DJ Afro.

Alpha Mwana Mtule
Image: HISANI

Mburudishaji na mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injili Peter Wangudi almaarufu Alpha Mwana Mtule hatimaye amekuwa mtu huru baada ya kuachiliwa kutoka Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ambako inadaiwa alikuwa akizuiliwa kwa wiki chache zilizopita kwa sababu ya salio kubwa la bili ambalo halikuwa  limelipwa.

Mwana Mtule aliruhusiwa kwenda nyumbani usiku wa kuamkia Jumanne baada ya mchekeshaji Eric Omondi kuwahamasisha Wakenya mtandaoni kuchangia salio la bili ya hospitali la takriban nusu milioni.

Kufuatia hayo, mwimbaji huyo wa nyimbo za injili anayejulikana sana kwa kumuiga DJ Afro alimshukuru Eric Omondi na Wakenya wote waliomsaidia kuachiliwa kutoka hospitalini.

“Asante Wakenya wote @ericomondi kwa kunisapoti. Sasa niko huru mmeniondolea salio la hospitali yangu manze nyi ni wasee wa maana sana,” Alpha Mwana Mtule alisema katika taarifa yake ya Jumanne asubuhi.

Ili kuthibitisha kuwa sasa yuko sawa na yuko tayari kurejea kwenye sanaa yake, aliambatanisha kauli yake na video yake akifanya sanaa yake maarufu ya kumuiga DJ Afro.

”Mungu awabariki nyote Nawapenda sana. Muendelee kusupport muziki wangu,” aliongeza.

Hapo awali mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alifichua kwamba hakuruhusiwa kutoka hospitalini hata baada ya kupona, kabla ya salio la Ksh 450,000 kulipwa.

Siku ya Jumatatu asubuhI, Eric Omondi alipiga hatua ya kuenda katika hospitaliya KNH ambako mwanamuziki huyo alikuwa amezuiliwa na kuwasihi Wakenya kumsaidia msanii mwenzake Alpha Mwana Mtule kulipa salio la bili.

Katika taarifa yake kwenye Instagram, mchekeshaji huyo ambaye pia anajihusisha pakubwa na uanaharakati alifichua kuwa licha ya kuruhusiwa kutoka hospitalini takriban mwezi mmoja uliopita, Mwana Mtule hawezi kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa sababu ya bili ya karibu shilingi nusu milioni.

“Huyu jamaa amepitia mengi kweli. TEAM SISI KWA SISI naomba tutoe hapa leo,” Eric Omondi alisema kupitia akaunti yake ya Instagram.

Aliongeza, "Aliruhusiwa kutoka hospitalini kama mwezi mmoja uliopita lakini anazuiliwa hapa kwa sababu ya bili isiyolipwa ya Ksh450k, hii tunaweza kuongeza saa hizi niende nimtoe aende nyumbani asikule Krismasi hapa. Namba yake ni 0725468373 (JINA: PETER WANGUDI). Tuma chochote unachoweza.”

Eric aliambatanisha taarifa yake na video yake akiwa na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili ambaye amekuwa mgonjwa kwa miezi michache iliyopita.

View Comments