In Summary

•Diamond ameashiria fahari yake kubwa baada ya mwanawe Prince Nillan kuhudhuria masomo ya Madrasa ili kupata mafundisho ya Kurani.

•Kusherehekea maendeleo ya mwanawe katika masomo ya Uislamu, Diamond alichapisha video hizo kwenye Instastori zake.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Siku ya Jumamosi, staa wa bongo fleva Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz aliashiria fahari yake kubwa baada ya mwanawe Prince Nillan kuhudhuria masomo ya Madrasa ili kupata mafundisho ya Kurani.

Katika ukurasa wake wa Instagram, bosi huyo wa WCB alichapisha video za mtoto huyo wake wa pili akipokea mafundisho ya Kurani kutoka kwa mwalimu wa Kiislamu na akionekana kuyafuatilia vizuri mafundisho hayo.

Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 7 pia alionekana akifundishwa kuomba na Kiarabu, na alionekana kuelewa na kuyafuata vizuri yale aliyokuwa akifundishwa na mwalimu wake.

Kusherehekea maendeleo ya mwanawe katika masomo ya Uislamu, msanii Diamond Platnumz alichapisha video hizo kwenye Instastori zake na kuambatanisha video hizo kwa emoji za moyo, ili kuonyesha upendo.

Prince Nillan ni mtoto wa pili wa Diamond Platnumz. Alizaliwa Desemba 2016, mwaka mmoja tu baada ya dada yake mkubwa Latifah Dangote.

Takriban miezi miwili iliyopita, staa huyo wa bongo alimtuliza mwanawe Prince Nillan baada ya kushindwa kuhudhuria sherehe ya siku yake ya kuzaliwa mnamo Desemba 6.

Katika taarifa yake ya mwezi Disemba bosi huyo wa lebo ya WCB alimtaka mtoto huyo wake wa pili wa mwanasosholaiti Zari Hassan asiwe na wasiwasi kuhusu yeye kutohudhuria sherehe yake kwani anapanga kulipa fidia.

Alisema ili kulipia kukosa karamu zilizopita, atawaandalia tafrija kubwa kijana wa miaka saba na dada yake mkubwa Tiffah Dangote.

“Nimekosa siku yako maalum na ya dada yako mwaka huu mwanangu.. Ila usijali, nitawafanyia wote Birthday Party maalum kwa ajili yako na dada yako mtakapokuja kwa ajili ya mkesha wa mwaka mpya nchini Tanzania!!!,” Diamond alisema kupitia Instagram.

Staa huyo wa bongo fleva aliendelea kumhakikisha mwanaye na Zari kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Kumbuka Papa anakupenda sana @princenillan," alisema na kuambatanisha taarifa yake na picha ya mvulana huyo wa miaka saba.

Nillan na dadake Tiffah Dangote walikuwa nchini Tanzania kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba ambapo walipata fursa ya kushiriki muda na familia ya Diamond.

Wawili hao ambao ndio watoto wakubwa wa bosi huyo wa WCB walisafiri naye Tanzania kutoka Afrika Kusini wanakoishi na mama yao.

View Comments