In Summary

•Eric alitangaza kukamilika kwa daraja hilo la chuma siku ya Alhamisi asubuhi na akaonyesha video ya msichana huyo wa shule akiifungua rasmi.

•Mchekeshaji huyo alitoa wito kwa Wakenya kusaidia kujenga daraja jipya katika eneo hilo katikati mwa mwezi Januari.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi amekamilisha ujenzi wa daraja jipya kuchukua nafasi ya daraja hatari ambalo msichana mdogo aliyetambulika kama Kemunto alirekodiwa akivuka mwezi uliopita

Eric alitangaza kukamilika kwa daraja hilo la chuma siku ya Alhamisi asubuhi na akaonyesha video ya msichana huyo wa shule akiifungua rasmi.

Huku akitangaza mafanikio hayo makubwa, Eric alimsherehekea Kemunto akisema kwamba alibadilisha jamii nzima. Alilipa daraja lile jina lake.

“KEMUNTO BRIDGE IMEKWISHA. Msichana huyu mdogo amebadilisha Jumuiya nzima. Yeye ni Shujaa. Daraja hili sio la Kihistoria pekee bali pia ni la KISHARA sana,” Eric Omondi alitangaza kupitia mtandao wa Instagram.

Aliongeza, “Inaashiria azimio la watu, INAFANIKISHA nguvu katika UMOJA!!! Kwamba Wakenya wanaweza kuja pamoja na KUTATUA matatizo yao. TUNAZIBA MAPENGO. Mapengo kati ya MASIKINI na MATAJIRI lazima na yanaweza kupunguzwa na kupungua. TUNAZIBA Mapengo yaliyoundwa na Migawanyiko ya Kisiasa na Kikabila. TEAM SISI KWA SISI HAKUNA LISILOWEZEKANA!!! KWA PAMOJA KILA KITU KINAPATIKANA!!!”

Mchekeshaji huyo alitoa wito kwa Wakenya kusaidia kujenga daraja jipya katika eneo hilo katikati mwa mwezi Januari baada ya msichana mdogo aliyetambulika kama Kemunto kurekodiwa akivuka daraja hatari juu ya mto huo uliofurika.

Mnamo Januari 17, Eri alishiriki video yake akiwa kwenye daraja ambayo alinuia kusaidia katika kuijenga upya na akafunguka kuhusu mambo ya kukatisha tamaa aliyoyaona hapo.

"Leo nilishuhudia mama akiwa amembeba mtoto wake wa miezi 3 akivuka "Daraja la Kifo", niliona watoto wa umri wa mwaka 1 na nusu wakivuka mtego huu wa kifo. Wanawake wakibeba mitungi huku wakichunga maisha yao wenyewe,” Eric Omondi alisema chini ya video aliyoshiriki kwenye Instagram.

Kabla ya kulipata daraja hilo hata hivyo, alikuwa amepotoshwa hapo awali na kuonyeshwa daraja lingine hatari

Licha ya kupotoshwa hapo awali, Eric alisema kuwa bado atasaidia kujenga daraja alilokuwa ameonyeshwa hapo awali pamoja na lile halisi.

"Tulipata Daraja halisi lakini pia tutajenga Daraja hilo lingine pia kwa sababu wao pia wanalihitaji," alisema.

Kupatikana kwa daraja hilo halisi kumekuja baada ya mwanahabari wa mtandaoni kufanya mahojiano na mzazi wa mtoto halisi aliyerekodiwa akivuka daraja hilo hatari.

“Mahali Eric Omondi ameenda, huyo mtoto anaitwa Shirleen sio huyo. Huyu mtoto wangu anaitwa Ann Kemunto Ondavu. Na mimi naitwa Thomas Ondavu Obure. Yule mtoto ndiye huyu,” baba wa mtoto halisi alisema kwenye mahojiano.

Alifichua kuwa watoto wengi huvuka na watu wazima huvuka daraja kila siku wakielekea shuleni, kanisani na sehemu zingine muhimu.

View Comments