Mwimbaji mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji ameendelea kumuomboleza kwa uchungu mwanawe Jazeel Adam aliyefariki takriban miezi mitatu iliyopita.
Jazeel, ambaye alikuwa na umri wa miaka mitatu tu alipofariki, alipoteza maisha yake mnamo Desemba 25 mwaka jana kufuatia ajali iliyotokea katika hoteli aliyokuwa akikaa na familia yake. Alikuwa mtoto wa pili wa msanii huyo wa kundi la Neccesary Noize.
Siku ya Alhamisi, rapa huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha ya chumba tupu ndani ya nyumba yake na kufunguka jinsi anavyokosa uwepo wa mvulana huyo mdogo.
"Kimya ni kikubwa sana mpenzi wangu @jazeeladam, haswa katika sehemu yetu maalum. Nakutafuta kila mahali mvulana wangu, kila mahali,” Nazizi aliandika kwenye picha hiyo.
Katika chapisho jingine, alishiriki picha ya kumbukumbu iliyomuonyesha akiwa na mumewe na mtoto wao marehemu na chini yake akafunguka kuhusu huzuni anayohisi.
"Ninakufa, ninaumia sana, siwezi kuvumilia," aliandika na kuambatanisha ujumbe huo na emoji ya uso unaolia.
Hizi zilikuwa jumbe za hivi punde zaidi ambazo msanii wa bendi ya Neccesary Noize ameshiriki tangu kifo cha mwanawe mnamo siku ya Krismasi. Mara kadhaa, katika siku zilizopita ametumia ukurasa wake wa Instagram kumuomboleza mvulana huyo wa miaka mitatu na kueleza uchungu ambao anahisi.
Siku ya Jumatano, alikumbuka alivyokuwa akitumia jioni zake na mwanawe huyo, wakitazama programu ya watoto, kucheka pamoja na kukumbatiana. Alitaja nyakati za jioni kuwa nyakati alizopenda zaidi kwa siku.
"Ilikuwa wakati wangu niliopenda sana kwa siku ambapo tulipumzika na kutazama paw patrol na kucheka na kukumbatiana," Nazizi aliandika kwenye Instagram.
Aliambatanisha ujumbe wake na video fupi iliyoonyesha akilia huku akitazama picha ya marehemu mwanawe iliyowekwa ukutani.
Aliendelea kufunguka jinsi anavyomkosa mwanae, na jinsi anavyolia kila jioni akikumbuka kuwa mtoto huyo hayupo naye tena.
"Sasa umeenda kijana wangu, mama hana mtu wa kukaa naye jioni na mimi hulia na kulia nikitamani ungekuwa hapa," alisema.
Mapema mwezi huu, msanii huyo alidokeza kuwa ametumia takriban miezi miwili na nusu iliyopita akiwa amejifungia ndani ya nyumba yake kufuatia kifo cha mwanawe.
Katika taarifa yake, mwimbaji huyo wa kundi la Necessary Noize aliwashukuru wale ambao wamekuwa wakimtia moyo kuondoka nyumbani na kuungana tena na ulimwengu lakini akadokeza kuwa haijakuwa rahisi kwake tangu mwisho wa mwaka jana.
"Kwa kila mtu anayenitia moyo nitoke nyumbani.. asante lakini, imepita miezi 2 na nusu ya vita hivi..," Nazizi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha ujumbe wake na meme inayoelezea jinsi wakati mwingine anahisi huzuni sana kuondoka nyumbani na nyakati nyingine anahisi kuondoka nyumbani kunaweza kupunguza huzuni yake.
"Vita kwenye ubongo.. Kuhisi huzuni sana kuondoka nyumbani ... Kujua kwamba kwenda nje kutafanya nihisi huzuni imeshuka chini," meme aliyoposti ilisema.