In Summary

•Habari za kifo cha mtangazaji huyo mahiri ziliibuka Jumanne asubuhi, siku chache tu baada ya kuripotiwa kuwa amelazwa hospitalini.

•Jahmby amekuwa akipambana na ugonjwa wa Thoracic Endometriosis kwa muda mrefu na amelazwa hospitalini mara kadhaa.

Mtangazaji Jahmby Koikai ameaga dunia.
Image: HISANI

Mtangazaji maarufu wa mziki wa reggae Mary Njambi Koikai almaarufu Fyah Mummah Jahmby amefariki.

Njambi alifariki katika Hospitali ya Nairobi siku ya Jumatatu, mwendo wa saa tatu usiku baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alikuwa amelazwa katika ICU.

Habari za kifo cha mtangazaji huyo mahiri ziligonga vichwa vya habari Jumanne asubuhi, siku chache tu baada ya kuripotiwa kuwa amelazwa hospitalini.

Wiki iliyopita, Jahmby alilazwa katika Hospitali ya Nairobi na alituma ombi la damu aina ya  O positive.

"Habari familia, kwa sasa nimelazwa katika wadi ya pioneer ya hospitali ya Nairobi na ninahitaji Blood O positive. Tafadhali naomba wafadhili wa damu kwa Mary Njambi Koikai," posti iliyowekwa kwenye Instastori zake ilisoma. 

Jahmby amekuwa akipambana na ugonjwa wa Thoracic Endometriosis kwa muda mrefu na amelazwa hospitalini mara kadhaa.

Mapema mwaka huu, mtangazaji huyo alisimulia safari yake na ugonjwa wa endometriosis.

Fyah Mama, kama anavyojulikana sana alisema hali hiyo ilimfanya maisha yake ya ujana kuwa magumu. Alikuwa ameifanya kazi yake kuwaelimisha watu juu ya ugonjwa huo.

Huku akionyesha picha yake ya zamani miaka sita iliyopita, Jahmby alinukuu,"Siku kama hii, miaka 6 iliyopita, nilifanyiwa upasuaji wa kubadilisha maisha kutokana na ugonjwa huu wa mwili mzima. Hatukuwa na habari kwamba ugonjwa huo ulikuwa umeathiri moyo wangu, mgongo wangu, appendix yangu (iliyotolewa), meno yangu; ufizi wangu, mapafu yangu, na diaphragm yangu, iligunduliwa kuwa na upungufu mkubwa wa damu.

Haikuwa hadi tulipofika kwenye Kituo cha Huduma ya Endometriosis huko Atlanta, tulipopata kujua jinsi ugonjwa huu ulivyokuwa umeenea na uharibifu uliosababishwa kwenye pafu langu la kulia na diaphragm baada ya makumi ya upasuaji.

Macho yangu yaliathiriwa na hivi majuzi ilibidi nipate dawa mpya. Nimehuzunishwa na miaka mingi iliyochukua kugundua ugonjwa huu.

Kutokana na ucheleweshaji huu, ugonjwa huenea karibu kila sehemu ya mwili. Kufikia wakati tunatafuta matibabu maalum, sasa tunapaswa kukabiliana na magonjwa mengine ya kinga ya mwili yanayosababishwa na Endometriosis na Adenomyosis."

Jahmby aliongeza kuwa nchini Kenya idadi ya watu walio na ugonjwa wa endometriosis ni kubwa zaidi

"Jaribu hii hesabu ya wanawake au wasichana 10 unaowafahamu, 1 kati yao ana maumivu makali ya hedhi ambayo yanaweza kuwa Endometriosis. Na huku kwetu Kenya inaonekana idadi ni kubwa zaidi. Kwa hiyo zaidi ya wanawake milioni 200 duniani kote wanapambana na Endometriosis. Machi ni Mwezi wa Endometriosis Duniani. "

Aliendelea kuongeza kuwa waathiriwa hushuhudia dalili tofauti.

"Tunahitaji mbinu mbalimbali za kutambua ugonjwa huu na kutibu haraka iwezekanavyo. Ndio mara tu vijana wanapolalamika kwa maumivu mengi ya hedhi na kuonyesha dalili zote zinazohusiana na ugonjwa huu wa kutisha, basi wanapaswa kutibiwa na wataalamu mara moja," alisema.

Kwa kumalizia, Jahmby aliongeza kuwa hawezi kueleza maumivu ambayo ugonjwa huo ulimwekea kwa maneno.

"Ugonjwa huu pia unaweza kuwapata wanawake baada ya kujifungua na wale wanaokoma hedhi. Nilipata utambuzi baada ya miaka 19 ya kuishi katika maumivu makali. Siwezi kukuelezea niliyopitia kwa sababu ninakosa maneno. Kijana wangu. Miaka yangu ya ishirini- 30 haikuwa rahisi sana kutibu na baada ya kupona inahitaji utunzaji mwingi," alisema.

Mungu ailaze roho ya Jahmby mahali pema peponi!!!

View Comments