In Summary

•Ondiek ameandika ujumbe wa hisia, siku moja tu baada ya kuzikwa kwa mke wa muigizaji mwenzake Matayo Keya almaarufu Alphonse Makokha.

•Muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alimuomboleza marehemu Purity Wambui na kutaka roho yake kupumzika kwa amani.

Image: FACEBOOK// ONDIEK NYUKA KWOTA

Muigizaji mkongwe wa kipindi cha Vioja Mahakamani Hiram Mungai almaarufu Ondiek Nyuka Kwota ameandika ujumbe wa hisia, siku moja tu baada ya kuzikwa kwa mke wa muigizaji mwenzake Matayo Keya almaarufu Alphonse Makokha.

Katika ujumbe wake wa Jumanne mchana, muigizaji huyo mcheshi alizungumza kuhusu maumivu ya Makokha baada ya kumpoteza mke wake ambaye amekuwa naye kwa takriban miongo mitatu.

Ondiek alizungumza kuhusu jinsi ilivyo vigumu kukabiliana na majonzi baada ya kifo cha mtu ambaye mtu ameshiriki naye mengi na kuunda kumbukumbu nyingi naye.

"Haijawahi kuwa rahisi kusema" kwaheri ya mwisho" kwa mpenzi wako wa miaka 30. Uzito wa kumbukumbu zinazoshirikiwa, uhusiano uliokua kwa miongo kadhaa ya heka heka, na muunganisho wa kina unaoimarika kadiri wakati unavyofanya kuaga kama hii kuwa ngumu sana,” Ondiek alisema kupitia mtandao wa Facebook.

Aliongeza, "Uchungu wa kutengana na mtu ambaye amekuwa sehemu muhimu ya maisha yako kwa muda mrefu hauwezi kupimika, unagusa kila kona ya moyo na roho yako."

Muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alimuomboleza marehemu Purity Wambui na kutaka roho yake kupumzika kwa amani.

“Pepea pamoja na malaika Purity hadi tukutane tena. Safari yako iwe ya amani na roho yako ipate utulivu kati ya nyota, hadi njia zetu zikutane tena," alisema.

Ondiek aliambatanisha ujumbe wake na picha zilizopigwa wakati wa mazishi ya marehemu aliyezikwa Alhamisi, Juni 13, katika Makaburi ya Lang’ata, Nairobi.

Mke wa Makokha, marehemu Purity Wambui alipoteza maisha mnamo Juni 1, 2024 baada ya kuugua saratani ya matiti kwa muda mrefu.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Tuko Kenya, muigizaji Makokha alifichua kuwa mkewe alifariki akiwa nyumbani. Alisema kuwa marehemu alikuwa chini ya uangalizi wa binti yao wakati alifariki.

“Nilikuwa naenda kazini. Nilikuwa nimewacha binti yangu nikamwambia amuangalie mama yake, naenda kutafuta riziki,” alisimulia.

Alifichua kuwa ni muigizaji mwenzake Hiram Mungai almaarufu Ondiek Nyuka Kwota ambaye alifahamishwa wa mara ya kwanza kuhusu kufariki kwa mkewe.

Ondiek kisha akamjulisha kuhusu habari hizo za kusikitisha kwa njia ya huruma.

“Nililia kwa muda wa saa mbili hivi. Mimi ndiye nilikuwa nikiendesha gari, yeye (Ondiek) alichukua usukani na kuendesha. Nikasema kwa sababu imefanyika, tuendelee na safari. Nikaenda kazini tu kama kawaida. Hiyo siku tulikuwa tulale lakini ata sikulala, lazima ningerudi. Mungu alinipatia nguvu nikawapeleka nyumbani vizuri, pia mimi nikafika nyumbani vizuri,” alisema.

Makokha alisema tukio hilo la kusikitisha limeacha jeraha kubwa ambalo hana uhakika kama litapona.

“Inauma, inauma. Ni uchungu kwa sababu sitakuwa tena na jiko yangu karibu ambayo nilikuwa naipenda,” alisema kwa uchungu mwingi.

View Comments