In Summary

•Gidi alipata nafasi ya kuingia uwanjani Stade de France ambako alishuhudia mashindano mbalimbali ambayo Kenya ilikuwa ikishiriki.

•Mtangazaji huyo mahiri wa redio alifichua kuwa walitozwa takriban Sh75,000 kwa kila mtu ili kutazama mbio.

Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Ilikuwa ni wakati wa kujivunia mtangazaji wa Radio Jambo, Gidi Ogidi, aliposhuhudia moja kwa moja Michezo ya Olimpiki ya 2024 inayoendelea jijini Paris, Ufaransa.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha asubuhi aliondoka nchini Kenya kuelekea Ufaransa wiki iliyopita na Jumapili jioni, alipata nafasi ya kuingia uwanjani Stade de France ambako alishuhudia mashindano mbalimbali ambayo Kenya ilikuwa ikishiriki. Aliandamana na familia yake kwa siku hiyo kubwa.

"Mapema ndio best zaidi, nyakati za kihistoria katika Stade de France kushangilia #TeamKenya. LETS GO KENYA, LETS GO,” Gidi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram alipofika uwanjani Jumapili.

Aliambatanisha taarifa yake na picha zake na familia yake wakiwa uwanjani na ratiba ya matukio ya Jumapili jioni.

Katika taarifa nyingine, mtangazaji huyo mahiri wa redio alifichua kuwa walitozwa takriban Sh75,000 kwa kila mtu ili kutazama mbio.

"Tiketi ya bei nafuu zaidi inayopatikana kwa fainali za leo za Olimpiki za 100m Wanaume katika Stade de France ni Euro 525, hiyo ni Ksh75,000 kwa kila mtu, Weuh!" alisema.

Pia alipata nafasi ya kutangamana na timu ya wanawake ya voliboli ya Kenya katika Kenya House nchini Ufaransa kabla ya kuingia uwanjani kuishangilia timu.

“Nimemuona Omanyala ndiye anafuata,” aliandika chini ya picha ya bingwa wa mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala.

Kwa bahati mbaya, Omanyala hakufuzu kwa fainali ya mbio za mita 100 kwani alitolewa katika hatua ya nusu fainali.

Alimaliza nambari nane katika kundi lake la nusu fainali, kumaanisha kwamba hangeshiriki fainali.

Noah Lyles wa Marekani alifanikiwa kushinda fainali hizo, Kishane Thompson wa Jamaica akiibuka wa pili naye Fred Kerley wa Marekani akiwa wa tatu.

View Comments