Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o amesikitika kuhusu kuhudhuria mazishi mengi nyumbani katika siku za hivi majuzi.
Katika chapisho la Jumamosi, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alifichua kuwa katika muda wa mwezi mmoja uliopita, amekuwa akienda nyumbani kwa ajili ya kuhudhuria mazishi kila wikendi.
Jalang’o alizungumza kuhusu jinsi amechoka kuomboleza kila mara na akamuomba Mungu arudishe nyakati za sherehe.
“Mwezi mmoja uliopita umekuwa mzito, kila wikendi nimesafiri kwenda nyumbani kwa mazishi. Mungu akomeshe, nirudishe kwenye sherehe, siwezi kuomboleza tena,” Jalang’o aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.
Mbunge huyo alifanya maombi hayo alipokuwa amehudhuria mazishi ya marehemu Marie Black Achieng’, binti ya muigizaji Nyaboke Moraa na Dkt Blak Aende.
Mwanasiasa huyo pia aliwapa pole familia hiyo, akawatakia amani na kuiombea roho ya Marie ipumzike kwa amani.
“Hakuna baba anapaswa kuzika watoto wao, Pumzika vizuri Marie. Dkt Black Aende na Nyaboke Moraa, Mungu awape amani,” Jalang’o aliandika.
Aliambatanisha ujumbe wake na pambo la mviringo lenye picha ya marehemu Marie.
Mwili wa bintiye Nyaboke Moraa uliondoka Nairobi kuelekea Kisumu siku ya Ijumaa, Agosti 9, kabla ya maziko kufanyika leo Jumamosi, Agosti 10 katika eneo la Kadongo, kaunti ya Kisumu.
Ibada ya kumkumbuka marehemu Marie ilifanyika katika kanisa la t CITAM, Embakasi siku ya Jumatano wakati Moraa alipokumbuka jinsi alivyojifungua mtoto huyo wake wa kwanza akiwa msichana mdogo sana.
Alisema kwamba alikuwa bado kijana mdogo wakati Marie alizaliwa na akabainisha kwamba walifanya kumbukumbu nyingi pamoja kabla ya kukutana na kifo chake mnamo Julai 28.
"Sijui jinsi ya kumuomboleza mtoto wangu, moyo wangu umevunjika. Moyo wangu umevunjika sana. Tulikuwa na kumbukumbu nzuri sana,” Moraa aliwaambia waombolezaji wenzake.
Aliongeza, “Moyo wangu umevunjika. sijui nitamuachilia aje mtoto wangu. Kuna wakati fulani maishani nilikuwa nikipitia mengi na alinikuta nimevunjika chumbani ananiambia ‘mum hukuwangi mtu mbaya, watu tu wako nawe ndio wabaya’.”
Muigizaji huyo mcheshi aliendelea kuzungumza kuhusu jinsi imekuwa vigumu sana kwake kukubali kuwa binti yake ameaga dunia.
“Marie alikuwa mtoto mzuri. Moyo wangu umevunjika *2. Sijui nitamwambiaje mtoto wangu aje apumzike kwa amani. Sina nguvu ya kumwambia mtoto wangu apumzike kwa amani. Bado siamini kuwa mtoto wangu amepumzika,” alisema Nyaboke kabla ya kuzidiwa na hisia.
Marrie Achieng, ambaye alikuwa mzaliwa wa kwanza wa Nyaboke Moraa alipoteza maisha katika hali isiyojulikana mnamo Jumapili, Julai 28.