In Summary

• DJ huyo anaweza kuonekana akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu na kwenye mkeka na hata kuzungumza vizuri huku akiburudika na wageni na familia.

•Tabasamu lake jipya lililopatikana, na mwili wake ulioboreka unaonekana sana kwenye video.

DJ Evolve
Image: HISANI

Video mpya imeonyesha maendeleo makubwa ya kiafya ambayo mtumbuizaji Felix Orinda almaarufu DJ Evolve amekuwa nayo takriban miaka minne baada ya tukio la kupigwa risasi ambalo lilimfanya apooze kiasi.

DJ Evolve aliachwa katika hali mbaya baada ya kupigwa risasi na Mbunge wa Embakasi Babu Owino katika klabu moja jijini Nairobi mnamo Januari 2020. Alilazwa hospitalini kwa miezi kadhaa kabla ya kuruhusiwa kuenda nyumbani Juni 2020 ili aendelee kupata nafuu kutoka nyumbani.

Jeraha alilopata lilimfanya apate matatizo ya kusimama, kutembea, kukaa chini na hata kuzungumza.

Katika video mpya iliyochapishwa na Brian Muchiri kwenye Tiktok, DJ huyo anaweza kuonekana akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu na kwenye mkeka na hata kuzungumza vizuri huku akiburudika na wageni na familia.

“Nimefurahi kukutana nanyi nyote,” anasikika akisema

Mtumbuizaji huyo pia anaweza kuonekana akifanya mazoezi ya mwili kwa usaidizi wa watu waliokuwa karibu naye, na alionekana kufurahia kuusogeza mwili wake.

Tabasamu lake jipya lililopatikana, na mwili wake ulioboreka unaonekana sana kwenye video.

Agosti mwaka jana, mahakama ilimuachilia mbunge Babu Owino katika kesi aliyoshtakiwa kwa kumpiga risasi DJ Evolve.

Wakati akizungumza na wanahabari nje ya mahakama baada ya uamuzi wa mwisho, mbunge huyo wa ODM alibainisha kuwa hukumu hiyo ilienda kulingana na matakwa ya Mungu.

Babu Owino hata hivyo alibainisha kuwa bado hajashinda katika kesi hiyo kwani kulingana naye, atashinda wakati DJ huyo hatimaye atafanikiwa kusimama na kutembea tena.

"Ninataka kumshukuru DJ Evolve (Felix Odhiambo Orinda), kwa kuwa rafiki yangu, kwa kuamini urafiki wetu na kwa kuwepo daima kwa ajili yangu," Babu Owino aliwaambia wanahabari siku ya Jumanne.

Aliongeza, “Hukumu hii imeenda jinsi Mungu Mwenyezi alivyotaka iende. Hivyo ndivyo Mungu alivyotaka iende. Nataka kusema, siku ambayo nitakuwa mshindi ni siku ambayo nitamuona DJ Evolve na kutembea, simama kando yangu."

Mbunge aliahidi kuendelea kumsaidia DJ Evolve  na kusimama naye hata baada ya kuondolewa mashtaka ya kumpiga risasi.

Aidha, aliahidi kumpeleka mtumbuizaji huyo nje ya nchi kwa matibabu maalum katika juhudi za kurudisha afya yake njema.

"Nitatembea pamoja na DJ Evolve, nitakuwa pale kwa ajili yake kila wakati. Kwa kweli ninapanga kumpeleka India kwa matibabu zaidi. Ninamwomba Mungu Mwenyezi ampe Felix nguvu zote za kimwili na za kiroho, za kumponya Felix na kuhakikisha kwamba anatembea katika siku za hivi karibuni,” alisema.

Babu Owino vilevile aliwashukuru mawakili wake kwa kusaidia katika kesi hiyo na pia familia yake kwa usaidizi wao na kwa kusimama naye katika kipindi cha miezi mingi ambayo kesi hiyo imechukua.

View Comments