In Summary

•Diamond aliibuka kuwa msanii aliyetazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube nchini Kenya akiwa na watazamaji zaidi ya milioni 123.

•Wimbo wa Injili wa Nina Siri wa Israel Mbonyi ndio wimbo uliotazamwa zaidi kwenye YouTube nchini Kenya.

Diamond Platnumz, Harmonize, Alikiba
Image: INSTAGRAM

Ni dhahiri kwamba idadi kubwa ya Wakenya huchagua kutazama muziki kutoka nchi jirani ya Tanzania badala ya muziki wa wasanii wa humu nchini.

Hii inaonekana katika ripoti ya hivi punde zaidi ya YouTube kwa mwaka mmoja uliopita kati ya Septemba 16, 2023 na Septemba 16, 2024.

Katika kipindi hicho, staa wa Bongo, Diamond Platnumz aliibuka kuwa msanii aliyetazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube nchini Kenya akiwa na watazamaji zaidi ya milioni 123.

Msanii wa zamani wa lebo ya Wasafi Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny aliibuka wa pili kwa kutazamwa kwenye YouTube baada ya kupata watazamaji zaidi ya milioni 81.

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ni wa tatu baada ya kutazamwa zaidi ya milioni 78 nchini Kenya katika kipindi hicho.

Zuchu ni msanii wa 4 wa Tanzania katika wasanii orodha ya watano bora akiwa na watazamaji zaidi ya milioni 78 kwenye jukwaa hilo la utiririshaji.

Msanii wa Injili Israel Mbonyi wa Rwanda ni wa tano katika orodha ya wasanii waliotazamwa zaidi kwenye YouTube nchini Kenya mwaka wa 2024 akiwa na watazamaji zaidi ya milioni 74.

Msanii wa Injili Peter Omwaka ndiye Mkenya wa kwanza kwenye orodha hiyo akiwa na watazamaji zaidi ya milioni 61 kutoka Kenya kwenye Youtube katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mbosso na Jay Melody wako nafasi ya 7 na 8 mfululizo kabla ya kundi la Kenya, Msanii Music Group, ambalo lilikuwa la 9 likiwa na watazamaji zaidi ya milioni 48.

Alikiba wa Tanzania anafunga orodha ya wasanii 10 bora waliotazamwa zaidi kwenye YouTube Kenyya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Staa wa Kenya Otile Brown aliingia katika nambari 15 akiwa na watazamaji zaidi ya milioni 41 kwenye jukwaa katika mwaka mmoja uliopita.

Wimbo wa Injili wa Nina Siri wa Israel Mbonyi ndio wimbo uliotazamwa zaidi kwenye YouTube nchini Kenya ukiwa na watazamaji milioni 37 kutoka nchini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Enjoy ya Jux na Diamond alishika nafasi ya pili huku Ibada ya Asubuhi ya Papi Clever na Dorcas ikishika nafasi ya tatu na wimbo wa Nitaamini wa Mbonyi ukiibuka wa nne.

View Comments