In Summary

• Anjella amezika tetesi za kuwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na bosi wa Konde Music Worldwide, Harmonize.

•Anjella alikiri kuwa na kipindi kigumu sana baada ya kutimuliwa katika lebo ya Kondegang mwaka jana.

Anjella na Harmonize
Image: HISANI

Aliyekuwa msanii wa Konde Music Worldwide, Angelina Samson almaarufu Anjella amezika tetesi za kuwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na bosi wa lebo hiyo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize.

Baada ya kuondoka kwake katika Kondegang miezi michache iliyopita, uvumi uliibuka kwamba Anjella alikuwa akichumbiana na bosi wake na hata alikuwa na ujauzito wake.

Hata hivyo, akizungumza kwenye mahojiano na Millard Ayo, malkia huyo wa muziki aliweka wazi kuwa hakuwahi kushiriki tendo la ndoa na Konde Boy.

"Hapana, Hapana, Hapana," Anjella alijibu alipoulizwa ikiwa aliwahi kuwa kwenye uhusiano na Harmonize, ikiwa alipata mimba yake na ikiwa bosi huyo wa Kondegang aliwahi kumtongoza akiwa katika lebo.

Anjella alikiri kuwa na kipindi kigumu sana baada ya kutimuliwa katika lebo ya Kondegang mwaka jana.

Alifichua kwamba alikuwa amepoteza matumaini kabisa na hata ilimbidi kutafuta usaidizi kutoka kwa mwanasaikolojia ili kukabiliana na changamoto ambazo alikuwa akipitia.

"Nilikaa na mwanasaikolojia kwa takriban miezi sita. Nilipoanza kuwa sawa ndio akaniambia sasa nianze kwenda studio. Kiukweli nilipitia wakati mgumu sana," Anjella alisimulia huku akibubujikwa na machozi.

Alikiri kwamba tetesi za uwongo za mitandaoni pia zilichangia katika hali ngumu aliyopitia kwani zilikuwa zikifanya azimie kila alipokumbana nazo hadi kufikia yeye kupokonywa simu na aliyekuwa akimsaidia.

Wakati wa mahojiano hayo, pia alizika tetesi kuwa aliyekuwa mpenzi wa Harmonize, Kajala Masanja ndiye aliyemfanya yeye na wasanii wengine waliokuwa wamesainiwa na lebo ya Konde Music Worldwide kutimuliwa.

Anjella aliweka wazi kuwa hafikirii kuwa mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang Harmonize ndiye aliyesababisha kukatizwa kwa mkataba wake na lebo hiyo.

"Sidhani, mimi sidhani," Anjella alijibu baada ya kuulizwa ikiwa muigizaji huyo mkongwe alihusika katika kutimuliwa kwake.

Malkia huyo wa muziki mwenye sauti nzuri aliweka wazi kwamba hakuwahi kuwa na uhusiano wa karibu sana na Kajala.

Alisema alikuwa akiwasiliana na muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 wakati tu hitaji la kikazi  lilipotokea.

"Kusema ukweli nilikuwa sina stori sana naye. Ilikuwa kukiwepo na jambo, naenda namwambia. Kama ni jambo fulani namwambia. Lakini hakukuwepo na yale mazoea ya kusema mnawasiliana labda," alisema.

View Comments