In Summary

•Kaka wa Ally B alitoa ombi la unyenyekevu kwa vituo vya redio na watumbuizaji kuacha kucheza nyimbo zake baada ya kifo chake.

•Kakake Ally B alieleza wanataka roho yake ipumzike kwa amani na kuwasihi wanaomkumbuka marehemu badala yake wamuombee.

Marehemu Ally B
Image: HISANI

Mwili wa mwanamuziki mkongwe mzaliwa wa pwani Ali Khamisi Mwaliguli almaarufu Ally B hatimaye ulizikwa siku ya Alhamisi, Novemba 2.

Ally alikata roho siku ya Jumatano alipokuwa akikimbizwa katika hospitali ya Coast General Teaching and Referral Hospital mjini Mombasa. Alikuwa akipambana na ugonjwa wa nimonia kwa siku kadhaa, kaka yake Mohamed Ramadhan alifichua.

Marehemu alifanyiwa ibada ya mazishi ya Kiislamu kabla ya mwili wake kuzikwa katika eneo la Maziara ya Cobra katika mtaa wa Mishomoroni, Kaunti ya Mombasa.

Watu mashuhuri, wanasiasa, mashabiki ni miongoni mwa walioungana na familia, majirani na marafiki wa marehemu mwimbaji huyo kumzika.

Wakati akitoa hotuba yake, kaka wa Ally B alitoa ombi la unyenyekevu kwa vituo vya redio na watumbuizaji kuacha kucheza nyimbo zake baada ya kifo chake.

“Tunaomba news anchors, radio presenters, ma-dj, tafadhali naomba, nyimbo za Ally msicheze. Tafadhali naomba,” kaka wa Ally B alisema.

Alieleza kuwa walitaka roho ya mwimbaji huyo ipumzike kwa amani na kuwaomba wanaotaka kumkumbuka marehemu badala yake wamuombee.

“Mcheze miziki yake tena. Kwa niaba  yake, naomba iwe anayetaka akimkumbuka amtilie dua. Lakini msipige miziki yake, tafadhali. Twaomba. Nyimbo zake tosha. Mimi kama ndugu yake nimesema,” alisema.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, muziki una nadhibitiwa maudhui ya nyimbo hayapaswi kuwa kinyume na maadili na mafundisho ya Uislamu au kuambatana na mambo mengine yaliyoharamishwa katika Uislamu kama vile pombe.

Mwanamuziki Ally B ambaye alivuma sana sana kwa nyimbo zake maarufu kama vile ‘Maria’ na ‘Bembea’ alitangazwa kufariki katika hospitali ya Coast General Teaching and Referral Hospital mjini Mombasa siku ya Jumatano alasiri ambapo alikimbizwa baada ya kulalamika kuhusu maumivu.  

Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa alifariki kutokana na ugonjwa wa pneumonia

Iliripotiwa kuwa mwanamuziki huyo ambaye tasnia yake ilivuma sana mwanzoni mwa miaka ya 2000 alifika nyumbani akiwa hana raha siku ya Jumatano alasiri na alikimbizwa hospitalini ambapo kwa bahati mbaya alifariki.

Rais William Ruto aliongoza Wakenya katika kumuomboleza mwimbaji huyo mzaliwa wa pwani baada ya habari za kifo chake kuenea haraka kote nchini.

Rais alimtaja kuwa mwanamuziki aliyekuza umoja katika jamii.

"Ninaungana na wanamuziki kuomboleza kifo cha Ally B, mwanamuziki aliyetumia talanta yake kukuza umoja na utangamano katika jamii yetu," Ruto alisema.

Aliongeza "Ali Khamisi Mwaliguli aliandika ujumbe wake wa amani ndani ya mioyo yetu, na tutaubeba daima wimbo huo wa maana. Mungu awape faraja familia yake, marafiki na mashabiki wake waliojitolea."

Wasanii wenzake na watu wengine mashuhuri wakiwemo Akothee, Nyota Ndogo, King Kaka, Lulu Hassan, Masauti, Jua Cali, Mike Sonko, Daddy Owen pia waliungana na Wakenya kuomboleza kifo chake.

View Comments