In Summary

•Omusula aliomba usaidizi na kufichua kwamba amekuwa akiishi mtaani kwa zaidi ya mwongo mmoja baada ya kupoteza kazi yake ya ufundi miaka mingi iliyopita.

•Omusula alithibitisha kwamba alikuwa amepata kazi katika ofisi ya Mwale na alionyesha kufurahishwa kwake na maendeleo hayo.

Leonard Omusula alikutana na mbunge wa Butere Tindi Mwale
Image: FACEBOOK// TINDI MWALE

Leonard Omusula, mwanamume kutoka Butere, Mumias kwenye video maarufu ya ‘Jina hutaki’ amepata kazi serikalini baada ya hatima yake ya kuhuzunisha kufichuliwa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Vincent Mboya, Omusula ambaye sasa ana umri wa miaka 43 aliomba usaidizi na kufichua kwamba amekuwa akiishi mtaani kwa zaidi ya mwongo mmoja baada ya kupoteza kazi yake ya ufundi miaka mingi iliyopita.

"Mimi ni fundi jinsi unavyoniona hivi. Mtu anisaidie kupata kazi, kwa sababu kulala mitaani, na kuishi mitaani, hiyo si sehemu ya maisha yangu," Omusula alisema.

Baada ya kufichuliwa kwa hatima ya Omusula, Mbunge wa Butere Tindi Mwale alimtafuta mwanamume huyo mwenye sura maarufu, akapata chakula naye na kumnunulia mavazi.

Mwale pia alimpa jamaa huyo kutoka Butere suluhu la muda mrefu kwa kumpa kazi ya kuwa mjumbe katika Ofisi ya Butere Bungeni.

“Nilimfikia Leonard Omusula, mkazi wa mtaani ambaye video yake ilisambaa akiomba usaidizi. Nimempa kazi ya kuwa mjumbe wetu wa Ofisi ya Butere Bungeni,” Mwale alisema Alhamisi.

Alishiriki video zake akitumia wakati mzuri na Omusula.

Katika mojawapo ya video hizo, Omusula alithibitisha kwamba alikuwa amepata kazi katika ofisi ya Mwale na alionyesha kufurahishwa kwake na maendeleo hayo.

“Niko hapa na mheshimiwa Tindi Mwale, amenitafutia fursa ya kupata kazi Eneo Bunge la Butere hapa Bungeni Nairobi. Mimi ni mjumbe wa ofisi ya Tindi Mwale kwa sasa katika Ofisi ya Bunge, jumba la Continental,” Omusula alisema.

Omusula aliweka wazi kuwa hatarejea tena mtaani baada ya kupata kazi katika afisi za eneo bunge la Butere bungeni.

Leonard Omusula amekuwa akivuma baada ya klipu ya zamani yake kuibuka mtandaoni, ambapo alikuwa akifanya mahojiano na ripota wa K24 TV  miaka mingi iliyopita.

Katika mahojiano hayo, Omusula alitetea uraibu wake mkubwa wa pombe, huku akifafanua jinsi angetumia KSh100 alizokuwa nazo mfukoni wakati huo kununua pombe ya shilingi 40 na kusaza shilingi 60 za nauli.

Baada ya mahojiano, mwandishi alisahau kumuuliza jina lake, jambo lililomfanya Omusula kuuliza, "Jina hutaki?"

Hapo ndipo mwandishi alipomuuliza naye akajibu, "Leonard Omusula, kutoka Butere Mumias."

View Comments