Baizire Jean Marie, ni mzee mmoja mwenye umri wa miaka 90 ambaye hadithi yake imegonga vichwa vya habari katika sehemu nyingi za ukanda wa Afrika ya Kati baada ya hadithi yake akisimulia kwamba katika umri wake wote huo uliokwenda, hajawahi kuwa na mpenzi hata mmoja na wala hana nia ya kuwa na mpenzi wala mchumba.
Katika mahojiano na mkuza maudhui mmoja kwenye mtandao wa YouTube kwa jina AfriMax, Jean Marie alieleza kwamba yeye anaishi maisha yake kawaida tu na hatqa siku moja hajawahi kuwa na mpenzi wala kukutana kimwili na mwanamke yeyote kwa miaka yote tisini aliyoishi kwenye ramani ya dunia.
“Nimekuwa nikiishi katika Kijiji hiki kivyangu tu na sijawahi kuoa na wala sijawahi kutana kimwili na mwanamke yeyote,” alielezea katika video hiyo.
Msimulizi anazidi kuhadithia kwamba baada ya kumdadisi mzee huyo kwa kina, aligundua kwamba wakati wa ujana wake alikuwa na ndoto ya kutaka kuoa na mpaka alikuwa anafanya karata za kuwafuata wanawake ila aghalabu akawa yeye ndiye anakataliwa, jambo ambalo huendqa ndilo lilififisha matumaini yake ya kuwa na familia na kuamua kuishi katika hali ya ukapera uliopitiliza maisha yake yote.
“Licha ya kujaribu kutongoza wanawake mbalimbali lakini sikufanikiwa kushiriki mapenzi na hata mmoja wao na mpaka sasa mimi bado bikra,” Jean Marie mkaazi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alielezea.
Mzee huyo sasa anaishi kwa huruma ya watoto wa ndugu zake ambao kidogo ndio wanamsaidia katika kazi ndogo ndogo ila kazi nyingi kama kujipikia na kujiendea shambani hufanya mwenyewe kwani anaamini kwamba mwanaume lazima achakarike ndio ale.
Baadhi ya wakaazi katika Kijiji hicho na ambao wamekua wakiona mzee huyo wanahisi kwamba huenda ni mikosi fulani au ulozi ambao umeskumiwa kwa mzee Marie ambaye wanaeleza kwamba tangu ujana wake hakutaka kabisa kujihusisha na wanawake hata kidogo.