Mwanahabari Betty Kyallo amefunguka kuhusu jinsi alivyovunjwa moyo sana na mwanamume wa kutoka jamii ya waluo ambaye aliwahi kuchumbiana naye.
Betty alifunguka kuhusu tukio hilo alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa mashabiki wake kupitia chaneli yake ya mtandao wa YouTube.
Shabiki mmoja alimuuliza jinsi mtu anavyokabiliana na uchungu baada ya mahusiano kuisha.
"Mojawapo ya maswali ya kuchekesha ambayo nilipata, ni jinsi ya kupona baada ya kutengana, haswa baada ya kuvunjwa moyo na mwanaume mjaluo," Betty Kyallo alisema.
Mtangazaji huyo wa zamani wa habari za runinga aliendelea kueleza kuwa si rahisi kuendelea baada ya kuvunjwa moja na mpenzi kutoka jamii ya Waluo.
Wakati huo huo, alifunguka jinsi alivyoachwa na moyo wenye uchungu baada ya uhusiano wake na mwanamume kutoka upande wa ziwa kufika kikomo.
“Wacha niwaambie nyie, huponi! Wale watu wamejengwa kwa ajili yako usipate kupona. Nimechumbiana na Mluo mmoja. Kwa ufahamu wangu najua nilichumbiana na mwanaume mmoja tu MLuo. Wueh, kuvunjwa moyo kwenye steroids.Moyo unachukuliwa, unapondwa, unakanyagwa. Kuvunjwa moyo huko kunashinda tuzo," alisema Betty.
Alibainisha kuwa amevunjwa moyo mara nyingi katika maisha yake ambapo mara nyingi yeye ndiye anayemuacha mpenzi wake lakini alikiri wakati mwingine kuwa pia anaachwa.
Katika ushauri wake kwa watu waliovunjwa moyo, alisema kuwa watu wanapaswa kuwa tayari kupitia mchakato wa baada ya kuachana ili wapone.
"Mambo yote hayo, lazima uyapitie, lakini huwezi kusema mimi ni mshindi, mimi ni tofauti, hapana. Nahisi kuna mambo ambayo ni lazima uyapitie, uhisi vibaya, ujiulize mbona alikufanyia hivyo baada ya mambo yote ulimfanyia.
Mambo hayo, ni sawa kuyazungumzia. Ni sawa kushiriki. Ni sawa kulia, ni sawa kujisikia vibaya kuhusu hilo, ni sawa kuomboleza, ni sawa." Alisema.
Mama huyo wa binti mmoja hata hivyo aliwashauri watu kutozingatia sana kipindi cha kulia baada ya kuvunjwa moyo bali wajaribu mahusiano mengine.
“Jipe muda. Kama wewe ni mtu kama mimi wa kumove on chap chap, unajua unaenda chap chap kama umesahau. Lakini kama wewe ni watu ambao wanachukua muda kupona, chukua muda wako na ufanye ambayo yanakufanyia kazi. Usitorokee uchungu, uhisi ndiyo iishe. Kadri unavyopuuza ndiyo utaendelea kuhisi vibaya,” alisema.