In Summary

•DJ Fatxo amedokeza kuwa mahojiano hayo hayafanikiwa kutokana na msongamano wa magari ambao ulimfanya achelewe kufika.

•Fatxo alikanusha vikali madai ya kufutiliwa mbali kwa mahojiano hayo kutokana na malalamishi ya umma na kudai kuwa kulikuwa na maoni mazuri kutoka kwa mashabiki.

DJ Fatxo ndani ya ofisi za Radio Africa

Mwimbaji maarufu wa Mugithi Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo amekanusha madai ya kituo kimoja cha redio kwamba walifutilia mbali mahojiano naye siku ya Ijumaa kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa mashabiki.

Katika taarifa yake Jumatano asubuhi, mwanamuziki huyo alidokeza kuwa mahojiano hayo hayafanikiwa kutokana na msongamano wa magari ambao ulimfanya achelewe kufika.

Fatxo alikashifu taarifa ya awali iliyotolewa na kituo hicho cha redio siku ya Ijumaa akiitaja kuwa ya kupotosha na yenye nia mbaya.

“Ukweli ni kwamba kufutiliwa mbali huko kulitokana na ucheleweshaji usioepukika wa trafiki ambao ulisababisha DJ Fatxo kuchelewa kwa mahojiano yaliyopangwa. Kwa hiyo tunaona kusingiziwa kwa barua hiyo kuwa ni jambo lisilofaa na ni wazo mbovu. Inachukiza, inapotosha na ni bahati mbaya tu,” ilisema taarifa hiyo.

"Tunathamini sapoti ya mashabiki wetu na uhusiano ambao tumejenga na vyombo vya habari. Ni muhimu kwetu kwamba taarifa sahihi zifikishwe kwa umma. Ni jukumu kuu la vyombo vya habari kutoa taarifa na sio kupotosha.”

Mwimbaji huyo wa Mugithi alikanusha vikali madai ya kufutiliwa mbali kwa mahojiano hayo kutokana na malalamishi ya umma na kudai kuwa kulikuwa na maoni mazuri kutoka kwa mashabiki katika machapisho ya matangazo ya mahojiano hayo yaliyoshirikiwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ya kituo hicho cha redio.

Zaidi, aliongeza kuwa kabla ya mahojiano hayo yaliyofeli kufanyika, tayari alikuwa amefanya mahojiano mengine na shoo kadhaa zenye mafanikio kwingineko baada ya kurejea Kenya kutoka likizo.

Siku ya Ijumaa, stesheni hiyo ya redio ilishiriki taarifa ikisema walilazimika kufutilia mbali mahojiano yaliyopangwa na DJ Faxto kufuatia malalamishi mengi kutoka kwa mashabiki wao.

Kituo hicho, kwa lengo ya kuwafahamisha mashabiki kilitangaza kwamba wangemkaribisha msanii huyo kwenye shoo yao ya asubuhi mnamo Agosti 18 kuanzia saa moja asubuhi hadi mbili asubuhi. Mahojiano hayo hata hivyo hayakufanyika.

Katika taarifa yao ya baadaye, walikiri kuwa wamesikia malalamiko ya mashabiki wao kuhusu mahojiano hayo na kuwaweka mbele.

“Kituo kilighairi mahojiano na Lawrence Njuguna Wagura almaarufu DJ Faxto ambayo yaliratibiwa tarehe 18 kuanzia saa 7 asubuhi hadi saa nane asubuhi. Kama shirika, tunathamini wateja wetu, na kama wasikilizaji wetu, nyinyi ni wa kwanza!" ilisoma taarifa hiyo iliyotiwa saini na timu ya mawasiliano ya umma ya kituo hicho.

View Comments