In Summary

•Mwishoni mwa wiki jana, Mo aliandamana na familia yake kuelekea jijini Dubai ambako wamekuwa wakisherehekea pamoja.

•Alisema kuwa alipata fursa ya kuwa na wakati mzuri ambao amekuwa akitaka sana na familia yake kila wakati.

DJ Mo na familia yake jijini Dubai
Image: INSTAGRAM// DJ MO

Mcheza Santuri mashuhuri Samuel Muraya almaarufu DJ Mo amekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa siku kadhaa zilizopita.

Mwishoni mwa wiki jana, Mo aliandamana na familia yake kwa ziara jijini Dubai ambako wamekuwa wakijivinjari pamoja.

Huku akiadhimisha siku hiyo maalum katika maisha yake, Mo alielezea furaha yake kubwa kwa kuweza kuisherehekea na familia yake.

"Kheri ya kuzaliwa kwangu!! Ni siku yangu leo, nashukuru Mungu nimesherehekea na familia yangu Dubai," alisema siku ya Jumapili.

Mcheza santuri huyo alifichua kwamba ilikuwa ndoto yake na bintiye, Ladasha Wambui, kuzuru jiji la Dubai na kujionea mandhari yake ya kuvutia.

Alichapisha video inayomuonyesha akijivinjari na familia yake kwenye ufukwe wa bahari jijini humo na kufurahia safari ya jahazi.

"Ndoto imetimia!!!!! Siku ya kuzaliwa jijini Dubai katika Jahazi na mke. Wakati wa ufukweni na shughuli nyingi pia zilikuwa sehemu ya kifurushi tulichokuwa tumeomba 😍😍," alisema chini ya video aliyochapisha Jumanne.

Alisema kuwa alipata fursa ya kuwa na wakati mzuri ambao amekuwa akitaka sana na familia yake kila wakati.

"Utukufu kwa Mungu. Nimeongeza mwaka mmoja. Familia ndiyo kwanza!" alisema.

Mo pia alichukua fursa hiyo kuwashauri wazazi wengine kuwazoesha watoto wao kutembea maeneo mbalimbali wangali wadogo.

"Mwishowe, Watoto Hawatakumbuka toy nzuri ulizowanunulia, Watakumbuka Muda Uliotumia Pamoja nao😎," alisema.

Wanandoa Size 8 na DJ Moh walikuwa wamekatiza ndoa yao kwa muda mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka jana.

Size 8 ambaye ni mwimbaji wa injili aliripotiwa kugura ndoa yake na kuwachukua watoto wao baada ya penzi lake na Mo kuyumba.

Wawili hao hata hivyo walisuluhisha mzozo wao kwa usaidizi wa viongozi wa kanisa na kurudiana siku chache baadae.

View Comments