Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor amezidi kuwamezesha mahasidi wake wa kisiasa vidonge vyao kwa mwendo wa aste aste, akizidi kuwakera wale wasiomtaka kuonekana na rais William Ruto.
Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tikiti ya chama cha ODM amekuwa akitajwa kama muasi wa chama katika siku za hivi karibuni, haswa baada ya kuonekana akifanya kinyume na matakwa ya chama kwa upendeleo wa upande wa serikali ya UDA.
Jumanne usiku, Jalang’o alipakia picha yake akiwa ananong’onezeana na rais Ruto na kuwataka wasiompenda kuhifadhi picha hiyo kwa minajili ya siku za usoni, kwamba atakuja kuwashangaza sana.
“Hifafhi picha hii kwa siku zijazo...Ni Mungu pekee ndiye anayejua!” Jalang’o aliandika ujumbe mfupi amabo ulinuia kuwakereketa wale ambao wanahisi kwamba ameasi chama kilichompeleka bungeni.
Katika upande wa kutoa maoni, watu Zaidi ya elfu moja walifika wengi wakionekana kumzomea kwamba hatokuja kushinda uchaguzi mwingine kwa tikiti ya ODM baada ya kuonekana kushirikiana pakubwa na upande wa Kenya Kwanza ambao awali Azimio waliweka bayana kwamba hawawezi kuitambua kama serikali.
Ikumbukwe mapema mwaka huu, mbunge huyo pamoja na wenzake wengine walikiuka msimamo wa ODM na kuelekea ikulu kinyemela na kukutana na Ruto wakati ambapo Odinga na jeshi lake walikuwa katika mchakato wa kuandaa maandamano ya kupinga uongozi wa Ruto.
Mwezi jana pia, licha ya ODM na Azimio kutangaza msimamo wao mkali dhidi ya mswada wa edha wa 2023 uliokuwa unapigiwa upato na Kenya Kwanza, Jalang’o alikuwa mmoja wa wabunge wa mrengo huo ambao walikiuka msimamo na kupigia mswada huo kura, katika kile walisema ni kuwatafutia vijana kazi.
Kupakia picha hii kunakuja siku moja tu baada ya kutoa mwongozo wenye utata kuhusu jinsi ajira zitakavyopatikana kwa vijana wa eneobunge lake kupitia matamasha yanayoandaliwa kwenye kumbi zilizopo Lang’ata.
Jalang’o vile vile alizomewa vikali kudai kwamba hakuna mtu anaweza kuandaa tamasha katika eneobunge hilo kama hatoweza kutoa asilimia 50 za kazi kwa vijana wake.