Mwanaharakati wa haki za kibinadamu Boniface Mwangi amefichua kwamba yeye alizaliwa kama bado ni mwanaharakati na mpambanaji wa haki sawa.
Akizungumza na Oga Obinna, Mwangi ambaye juzi amesherehekea kufikisha umri wa miaka 40 alsiema kwamba katika harakati zake za usumbufu, alijipata amefungwa jela kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 11.
Alisema kwamba kilichosababisha yeye kufungwa jela ni kuwasumbua wazazi baada ya kutoroka nyumbani ili kutafuta uhuru wake mitaani mbali na wazazi.
“Mimi nilizaliwa kama mpambanaji, nilifungwa jela nikiwa na umri wa miaka 11. Nilikuwa nawasumbua wazazi. Nilitoroka kutoka nyumbani kwenda kuishi mitaani kama mtoto wa mitaani. Nilitiwa mbaroni nikapelekwa mahakamani na kuhukumiwa miaka 7 jela kwa marekebisho halafu nikafukuzwa kabisa kutoka kwenye shule ya marekebisho,” Mwangi alihadithia.
Mwangi alisema kwamba kilichosababisha kufukuzwa kutoka shule hiyo ya marekebisho ni baada ya kutumbua majipu ya mabaya ambayo yalikuwa yanaendelea kwenye shule hiyo.
“Nilianika kile ambacho kilikuwa kinaendelea kule. Kuna watoto ambao walikuwa wanadhulumiwa kingono, walikuwa wanatutumia sisi wafungwa ili kulima mashamba ya walimu, kufanyishwa kazi za sulubu… ilikuwa tu ni kama utumwa, niliwaanika na kufukuzwa,” alisema.
Mwangi alikiri kwamba hapo ndipo safari yake ya upigaji picha ilianzia kwani alipiga picha na kuanika maovu ya shule hiyo.
“Nilipiga picha, nilikuwa kama miaka 14 nikazipeleka kwa waziri wa masuala ya kinyumbani na wakazitumia kuchunguza kilichokuwa kikiendelea,” alisema.
Hata hivyo, Mwangi alisema kwamba yeye aliona tu wenzake wakidhulumiwa lakini kitendo hicho hakikuwahi tokea kwake kwa kile alisema kwamba yeye alikuwa ni kichwa ngumu na asiyetaka upuuzi kufanyika karibu na yeye.
Baada ya kufukuzwa katika shule ya marekebisho ya tabia, Mwangi alirudi mitaani na kuanzisha biashara ya uchuuzi wa bidhaa kidogo kidogo, akiwashangaza wengi kwamba hakuweza kuhudhuria masomo ya shule ya sekondari.
“Mimi sikuwahi kusoma shule ya upili lakini baadae nikiwa miaka yangu ya 20s nilikwenda chuo cha uanahabari wa kupiga picha. Kwa sababu nilipofukuzwa katika shule ya kurekebisha tabia nikiwa na umri wa miaka 14 huo ndio ulikuwa mwisho wa masomo yangu. Nilikwenda kuchuuza vitabu barabarani,” Mwangi alisema.