Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii Diamond Platnumz huenda akafungwa jela katika kesi ambayo kampuni yake ilishtakiwa kwa ukiukaji wa kanuni za haki miliki na haki shiriki mwaka 2013.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, Tale atasikia hatima yake Ijumaa hii wakati kesi dhidi yake itakapotajwa.
Babu Tale ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya TipTop Connection inayojihusisha na masuala ya burudani huenda akaingia mahabusu kutokana na kushindwa kumlipa mhadhiri wa Kiislamu Sheikh Hashim Mbonde fidia ya shilingi milioni 250 za kitanzania.
Mbonde anataarifiwa kufungua maombi katika mahakama kuu dhidi ya TipTop Connection na Babu Tale akiomba meneja huyo wa WCB Wasafi kufungwa kwa kushindwa kumlipa fidia hiyo.
Wakili wa Mbonde aliambia toleo la Mwananchi Jumatatu kwamba hakimu amesikiliza maombi ya mteja wake na anatarajiwa kutoa uamuzi siku ya Ijumaa.
Mwaka 2013, Sheikh Mbonde alifungua kesi ya madai dhidi ya kampuni hiyo akidai imlipe fidia ya shilingi milioni 750 kwa kosa la ukiukwaji wa hakimiliki kwa kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha sheria ya hakimiliki na hakishiriki.
Hata hivyo, jarida hilo lilipojaribu kumfikia wakili wa mbunge Babu Tale, alidinda kuzungumza akisema kwamab hana uhakika kuhusu tarehe ya kusikilizwa kwa kesi dhidi ya mteja wake.