Kwa mara ya kwanza, mashabiki wa Rhumba nchini Kenya wasio na uwezo wa kumudu tiketi za VIPwatapata nafasi adimu ya kufurahia shoo ya wenzao wa VIP katika shoo ya gwiji wa Rhumba, Koffi Olomide Desemba 9.
Awali, Olomide aliratibiwa kufanya shoo mbili tofauti ile ya VIP pekee ikiratibiwa kufanyika Desemba 9 huku ile ya mashabiki wa rasharasha ikiratibiwa kufanyika Desemba 9.
Lakini sasa waandaaji wa tafrija hiyo kubwa ya Rhumba kufunga mwaka wakishirikiana na Radio Africa Group wamefanya mabadiliko kiasi tu kwa kuunganisha shoo zote mbili kufanyika siku moja – Desemba 9.
Shoo ya Koffi Olomide itafanyika katika uwanja wa ASK Dome Showground Jamhuri katika barabara ya Ng’ong jijini Nairobi, sawa tu na ilivyoratibiwa awali.
Awali tuliripoti kwamba tikiti nyingi zilikuwa zimeuzwa zote – pengine hii ikiwa ni moja ya sababy ambayo ilifanya shoo zote mbili kuungansihwa kwa pamoja kama njia moja ya kumpa kila shabiki wa Rhumba nafasi adimu ya kupakua burudani moja kwa moja kutoka kwa Koffi Olomide akiwa bado freshi.
“Baada ya kutafakari kwa kina na kuboresha hali ya matumizi kwa jumla kwa hadhira yetu, tumeamua kuchanganya maonyesho ya VIP na mashabiki kuwa tukio moja la kuvutia. Tarehe mpya ya onyesho la pamoja ni Jumamosi, tarehe 9 Desemba 2023, na ukumbi unasalia kuwa ASK Dome @ Show Ground,” sehemu ya taarifa ya waandaaji ilisoma.
Ujio wa Koffi Olomide nchini umetajwa kuwa wa kipekee na unasubiriwa kwa hamu kuu na mashabiki wake, ikiwa ni kukosa kutua nchini kwa Zaidi ya miaka 5 kufuatia tukio lililoichafua taswira yake kwa umma 2016 wakati video ilivujishwa ikimuonesha akimsukuma jukwaani mrembo aliyetajwa kuwa mmoja wa waliokuwa wacheza densi wake.
Wiki mbili zilizopita, Koffi Olomide alifanya video kwenye mtandao wake wa Facebook na kuthibitisha ujio wake, akisema kwamba lengo lake kuu ni kuonesha mashabiki wake wa Kenya anaowatambua kama ‘ndugu zangu’ jinsi anavyowapenda katika shoo hiyo.
“Mopao anakuja Nairobi tarehe 8 na 9 Desemba. Itakuwa ni moto, nitakuwa narejea Kenya baada ya miaka mingi. Niliwamiss sana muda mrefu. Nataka kuwaonyesha kina cha mapenzi yangu kwenu,” Koffi alisema katika klipu hiyo.