Rapa maarufu wa HipHop ya Kiswahili kutoka Tanzania, Rosa Ree amejisherehekea kwa umahiri wake kimuziki wenye kiwango cha kutukuta, akijifananisha na mkali wa Reggae kutoka Jamaika, Bob Marley.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rosa Ree alisema kwamba kuna mtu alimwambia kuwa yeye ni Bob Marley wa kizazi cha sasa na kukubali kwamba tamko hilo lilimuingia barabara!
Yeye ni rapper mwenye talanta, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo ambaye ameweza kushawishi raia na sauti zake zenye nguvu.
"Kuna mtu alisema Rosa Ree ni Bob Marley wa kizazi hiki, nilihisi hivyo," alisema wakati akifanyia kampeni wimbo wake wa hivi punde alioutoa siku chache zilizopita, 'Blessed'.
Rosa Ree amefanya hatua muhimu katika safari yake, akishirikiana na wasanii wenye vipaji duniani kote. Ameshinda hata tuzo tofauti za muziki. Ni miongoni mwa rappers wa kike wanaofuatiliwa sana Afrika Mashariki.
Hivi majuzi, alitambuliwa na Tuzo za Grammys pamoja na Femi One wa Kenya na Sho Madjozi wa Afrika Kusini kwa muziki wao bora wa hip-pop ambao una mvuto barani Afrika.
Bob Marley alikuwa mwimbaji wa reggae wa Jamaika, mpiga gitaa, na mtunzi wa nyimbo. Alizingatiwa kama mmoja wa waanzilishi wa aina hiyo alipochanganya vipengele vya reggae, ska na rock katika muziki wake. Alifariki tarehe 11 Mei 1981 akiwa na umri wa miaka 36.