Msanii wa Uganda Bebe Cool amewaacha wengi vinywa wazi baada ya kudai kwamba hamruhusu mtu yeyote kumpa mkewe vyakula kama sukari na mchele.
Akizungumza katika mahojiano na msanii mwenza wa kike Juliana Kanyamozi, Bebe Cool alisema kwamba yeye kwa muda mrefu amekuwa akifuata mlo maalum usio na sukari kama njia moja ya kujirefushia maisha.
Alisema kwamba angependa na mkewe pia kuishi maisha marefu kwani hataki kusalia katika ujane, hivyo pia amemamua kumtoa katika vyakula vya sukari.
“Simruhusu mtu yeyote kumpa mke wangu sukari na mchele,” alisema Bebe Cool kwenye mahojiano hayo. Alisema wanafuata lishe moja na hii imemsaidia Zuena, mkewe kutohitaji kufanya mazoezi.
Alisema amefanya kazi kwa bidii na hataki kushindwa kufaidi matunda ya bidii yake kwa sababu ya afya mbaya.
Alisema yeye huepuka sukari na hali chakula cha wanga baada ya saa 7 usiku. Usiku, anakula kuku na samaki tu.
Alisema alizuia familia yake kufanya ununuzi wa vitu fulani kwa sababu itakuwa sio haki ikiwa angeishi muda mrefu na mke akafa mapema. "Nakaa ndani ya nyumba peke yangu!" alisema.