Rapa na mfanyibiashara King Kaka ametangaza nia yake ya kumaliza bifu lake la muda mrefu na mchungaji wa kanisa la Neno Evangelism Centre, James Maina Ng’ang’a.
Kupitia video ambayo msanii huyo alipakia mitandaoni, alieleza kwamba ni wakati wa kumaliza ugomvi wake na pasta Ng’ang’a baada ya kuzozana kisa video moja.
Itakumbukwa miaka michache nyuma, video ya Pasta Ng’ang’a akimtoa mapepo mwanamke mmoja ilisambaa, baada ya mwanamke huyo kudai kwamba pepo lake lilikuwa linaitwa ‘King Kaka’, pasta Ng’ang’a akiradidi kuwa ni pepo ‘Kang Kaka’.
Tukio hilo lililotokea kwenye madhabahu ya kanisa ya Neno ilionekana kutomfurahisha King Kaka ambaye alihisi kuchafuliwa jina kwenye jamii ikizingatiwa kwamba ni msanii maarufu.
Hata hivyo, ameamua kumeza hasira zote na kumualika Ng’ang’a katika uzinduzi wa filamu yake wiki ijayo, akisema kwamba you tayari kusameheana naye na hata kuhudhuria moja ya ibada za Jumapili kanisani Neno.
“Habari Wakenya, niko na mwaliko rasmi kwa rafiki yangu mzuri kabisa – kuanzia sasa nitakuwa namuita hivyo – Pasta Ng’ang’a. tumekuwa na kuzozana kwingi mitandaoni, nataka tumalize. Kwa hiyo ninakutumia mwaliko niko na uzinduzi wa filamu yangu Mei 17 huko Two Rivers, na ninakualika rasmi,” King Kaka alisema.
“Kwa hiyo kama unamjua Pasta Ng’ang’a ama kama yuko mtandaoni, mtumie hii video. Pasta Ng’ang’a, mimi ni yule uliita Kang Kaka, mimi ni ile pepo ulitoa kwa yule mama, na ndio mimi niko hapa leo na rasmi ninakualika kuja tuone sinema na hata tukimaliza, hiyo itakuwa Ijumaa, Jumapili naweza kuja pia Kanisani nione vile unafanya mambo, si ndio? Pasta Ng’ang’a karibu sana, na ukikuja uulizie Kang Kaka, nitakuwepo,” aliongeza.