Bosi wa lebo ya muziki ya Wcb Wasafi, Diamond Platnumz amefunguka kwamba ngoma ya Komasava ndio ngoma kubwa amewahi kutunga katika safari yake ya zaidi ya miaka 15 kwenye tasnia ya muziki.
Akizungumza na Adesope Olajide kwenye Tamasha la Afroland, msanii huyo alikiri kwamba wakati wa kutunga ngoma hiyo, alikua ni nzito lakini hakuwahi fikiria itakuja kuwa kubwa na pendwa hivi kote duniani.
Diamond alikiri kwamba ametunga ngoma nyingine kubwa lakini Komasava imefunuka zote na ni jambo la kujivunia kama msanii.
"Kama nitasema ukweli, nilijua ngoma hii ni nzito lakini sikuwahi fikiria itakuwa kubwa hivi kwa sababu wakati mwingine unatoka nje ya studio na unajua ngoma hii ni nzuri na watu wataipenda lakini sikudhani itapata ukubwa huu," alisema.
"Naweza sema hii Komasava ni moja ya ngoma kubwa zaidi nimewahi kutengeneza. Na kadri siku zinavyozodi kuenda ndivyo inazidi kuwa kubwa hata zaidi," aliongeza.
Msanii huyo alizungumzia hisia ya kuona wasanii wakubwa kote ulimwenguni wakiguswa na utunzi wake na hata kuruka ndani kwa kufanya dance challenge.
"Wakati mwingine naweza kuwa nimelala nikiamka naona kina Chris Brown wakiimba na kucheza densi, kina Jason Derulo,...wasanii wengine wakubwa, sikuwahi tarajia wimbo wangu utakuwa wa kuvutia kwa tasnia ya muziki."
"Kwangu hii ni baraka kubwa na ninashukuru kwa sababu kama msanii ungependa kufanya kitu fulani ambacho kinaweza kuteka anga duniani kote," alisema.