In Summary

• Monroe amesema kwamba muonekano huo tofauti hautomfanya kumchukia Kartel akisema kwamba wakati unampenda, mtu unampenda katika hali zote.

• "Ni sharti tumpende Vybz jinsi alivyo kwa sasa, jamaa hata hakuwa mtanashati, ni ngoma nzuri tu huwezi kumtenganisha nazo,” alisema.

VYBZ KARTEL NA HUDDAH MONROE
Image: HISANI

Mwanasosholaiti Huddah Monroe amedai kwamba sasa ameanza kumzoea mkali wa dancehall kutoka Jamaika, Vybz Kartel na muonekano wake mpya, takribani wiki mbili baada ya kuachiliwa kutoka jela.

Kartel, 48, aliachiliwa kutoka jela baada ya kuhudumia kifungo cha miaka 13 gerezani kutokana na kile mamlaka zilisema ni kudorora kwa hali yake ya afya.

Picha za msanii huyo baada ya kuwa mtu huru zimekuwa zikienezwa mitandaoni, huku akionekana na sura iliyofura tofauti na muonekano wake wa awali kabla ya kwenda jela.

Baadhi ya wataalamu wamenukuliwa wakidai kwamba msanii huyo anaugua ugonjwa wa Graves - hali ya mfumo wa kinga ambayo huathiri tezi. Husababisha mwili kutengeneza homoni nyingi za tezi.

Monroe amesema kwamba muonekano huo tofauti hautomfanya kumchukia Kartel akisema kwamba wakati unampenda, mtu unampenda katika hali zote.

“Sasa nimeanza kuzoea kichwa cha Vybz Kartel. Vybz Kartel maisha yangu yote, kama unampenda mtu Fulani, unampenda tu bila kujali chochote. Hawezi fanya chochote kibaya,” alisema.

Huddah aliendelea kuchapisha picha za Vybz Kartel za kitambo akidai kwamba hata hivyo hakuwa na muonekano mzuri hata kabla ya kuugua na kudai alikuwa anafanana mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya katika siku zake za mihangaiko.

“Mwalimu! Hajawahi hata hivyo kuwa na muonekano mzuri, alikuwa anakaa kama Salasya hizo siku za kuhangaika. Wakati huo alikuwa mweusi na maskini. Ni sharti tumpende Vybz jinsi alivyo kwa sasa, jamaa hata hakuwa mtanashati, ni ngoma nzuri tu huwezi kumtenganisha nazo,” alisema.

Awali tuliripoti kwamba msanii huyo alitangaza kufanya shoo yake ya kwanza ya moja kwa moja mwishoni mwa mwaka huu, miaka 13 baadaye.

 

View Comments