Mchekeshaji wa Kenya anayeishi Marekani, Elsa Majimbo amedai watu wanaoishi ughaibuni au mijini kutuma pesa kwa wanafamilia wanaoishi vijijini ni kupalilia uzembe wao.
Kupitia mtandao wa TikTok, Majimbo alisema kuwa hiyo ni tabia ambayo imekithiri kwa wanafamilia nyingi barani Afrika kwamba mtu anayeishi mjini au nje ya nchi ni haki yake kuwatumia pesa wanafamilia wanaoishi vijijini.
Kwa upande wake, Majimbo alisisitiza kwamba hilo ni jambo ambalo hatofanya hata siku moja, na kusema yuko tayari kumuacha mwanafamiia anayemuomba pesa kuteseka na njaa hadi kufa badala yake kumpa pesa.
“Kutuma pesa kwa watu wa familia pana nyumbani ni jambo ambalo ni la kawaida sana katika familia nyingi barani Afrika na ambalo nalichukia. Niliona babangu akifanya hivyo na ndugu zake, wazee wake na mimi hata sijui mtu yeyote wa familia pana.”
“Ni kama kila mtu katika familia, mradi tu uko na kazi, wanatarajia kuwa utagawa pesa zao kwa kila mmoja wao inavyofaa. Na hiyo ni hulka ambayo sitafanya, na nilishajua tayari kwamba siwezi fanya,” Majimbo alisema.
Mrembo huyo aliwashauri watu kujitokeza ili kutafutia familia zao badala ya kutegemea vya ndugu zao wanaohangaika kutafuta riziki mijini na nje ya nchi.
“Eti unanililia kuwa wanao wanakufa njaa. Ndio wanakufa njaa kutokana na uzembe wako. Badalla yake amka toka tafuta kazi. Kusema ukweli mimi siwezi endekeza tabia zako, hiyo ni wazi kwamba wewe ni mzembe zaidi kuwa hai, mimi nitakuacha ufe na njaa,” Majimbo alisisitiza.
Maoni yake yalivutia hisia mseto, baadhi wakikubaliana naye na wengine wakimsuta kwa kile walisema wanafanya vile kwa kutambua jinsi wazazi wao walijitoa kwa jino na ukucha kuwaelimisha maishani.