Pasta Size 8 kwa mara nyingine amerejelea maamuzi yake ya kushangaza wiki tatu zilizopita kuhusu kuanza safari ya maisha bila mume.
Katika video moja iliyoenezwa Jumamosi Agosti 17, Size 8, katike kile kilichoonekana kama ni kutetea maamuzi yake, alisema kuwa alilazimika kufanya hivyo kwa sababu hakuwa na chaguo lingine.
Mchungaji huyo ambaye pia ni msanii wa nyimbo za injili alisema kuwa alilazimika kuchukua maamuzi magumu ya kumuacha DJ Mo na kuanza safari ya matumaini mapya, ila akasisitiza kwamba upendo wake kwa baba ya wanawe bado upo mwingi tu!
"Simchukii Dj Mo, sasa hivi hata ukigusa moyo wangu utamuona Dj Mo kwa umbali akitokea kutokana na kina cha upendo nilio nao kwake," Size 8 alisema.
"Lakini mimi kufikia hatua ya kusema kwamba kutengana ndio dawa, ni vile sikuwa na chaguo lingine," mama wa watoto wawili aliongeza.
Itakumbukwa wiki 3 zilizopita, Size 8 hakutoa sababu yoyote ya kuachana na Mo, akisema tu kwamba ni mambo yalikataa.
"Wakati mwingine ndoa hufanya kazi kwa neema ya Mungu, na wakati mwingine haifanyi kazi, lakini yote kwa Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi," Size 8 alisema kupitia Instagram.
Aliongeza: "Nimeolewa kwa miaka 11 na sasa ninaanza safari ya kuwa mseja. Lakini Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi, nakuabudu wewe Yaweh!"
DJ Mo kwa upande wake hajanena lolote kuhusu tangazo lililotolewa na mke wake Ila wiki jana alizungumza kwa kiduchu tu akisema yeye walikuwa na maafikiano na mkewe kwamba hakuna kugusa simu ya mwingine.
Licha ya suala la kuachana kwao kuendelea kuchipuka upya na dhana tofauti, wengi bado wanaamini wawili hao ni suala la muda tu, watarudiana.