Judy Nyawira, mkewe Abel Mutua amefunguka msimamo wake ikiwa anaweza kubali kupata mtoto mwingine.
Katika kipindi cha kujibu maswali kwa mumewe, Mutua alimuuliza mkewe swali la utani akilenga kujua iwapo atakubali kuzaa mtoto mwingine ikiwa ataahidiwa burunguti kubwa la hela.
Hata hivyo, mama huyo wa mtoto mmoja aliweka wazi kwamba ukweli wake upo pale pale kwamba hawezi kubali kubeba ujauzito mwingine tena, miaka kadhaa baada ya kumzaa mwanao wa pekee, Mumbus.
“Umewekewa shilingi milioni 100 mezani, utakubali kuzaa mtoto mwingine?” Abel alimtupia swali.
“Kusema ukweli kabisa, hapana. Siwezi. Nafikiri huo ni ukurasa ambao niliufunga kabisa na sidhani pesa inaweza badilisha,” Nyawira alisema.
Mutua aliongeza dau hadi milioni 200 lakini bado jibu la Nyawira lilisalia kuwa ‘HAPANA’.
“Jibu langu bado litasalia kuwa hapana, najua inasikika kama ‘lakini si uko na pesa za kumlea’ lakini unajua hiyo sio pointi. Ndio niko na pesa sasa hivi, lakini sidhani,” alisema.
Mwisho wa siku, Mutua alikubaliana na mkewe lakini akakiri yeye akipewa Sh500m kuongeza mtoto mwingine atakubali tu akisema kwamba kwake presha si nzito kama kwa Nyawira.
“Kwangu mimi ni sawa tu kwa sababu naona presha si nyingi kama kwako. Juu unajua majukumu mengi ya mwanamume ni huyu mtoto akuwe sawa, na sasa nikiwa na sh500m, tutaandika kila mtu, hata mfanyikazi atakuwa na naibu wake. Tutaunda ajira,” Mutua alisema.