Msanii Vivianne amewashangaza wengi wa mashabiki wake baada ya kufanya video yenye hisia kali za uchungu akieleza sababu zake za kufikia uamuzi wa kuukana Ukristo.
Kupitia Instagram yake, Vivianne alieleza kwamba hafikirii ana sababu nyingine tena ya kumfanya kuamini katika Ukristo kutokana na machungu ambayo amekuwa akiyapitia kimaisha.
“Naweza waambia ni kwa nini siamini tena katika Ukristo? Sidhani kama nina chaguo. Misingi ya Ukristo ni udhibiti na woga. Ni kuishi maisha yangu yote kutokana na maandiko kwenye kitabu. Maamuzi yako yote na kila kitu kukuhusu wewe vinaamuliwa na kitabu…”
Vivianne alisema kwamba watu wengi wamekuwa wakitumia kitabu hicho [Biblia] kuwafanyia wengine mabaya na kisha kutoroka na kujiridhisha na maandishi kutoka kwa kitabu hicho kuhusu vitendo vyao kwa wengine.
“Ninaamini katika nguvu za roho zetu, nguvu za uumbaji, ninaamini kwamba sisi ni miongoni mwa dunia nzima, sisi wote tumeunganishwa. Ninaamini kwamba binadamu ni kiumbe mwenye nguvu kwa sababu naamini ndani mwetu kila mmoja ana miungu wake.”
Msanii huyo anaeleza zaidi kwamba kinachomfanya kuchukia Ukristo hata zaidi ni jinsi Biblia inamuelezea mwanamke kama kiumbe aliyefikiriwa baadae, baada ya kila kitu – akiwemo mwanamume – kuumbwa.
“Kitabu hiki kinamfanya mwanamke kuwa wazo la baadae. Kwa sababu mwanamume aliumba kisha baadae mwanamke akaumbwa ili kumhudumia mwanamume. Hali ya kuwa ni mwanamke anayeleta uhai duniani. Hivyo ni vipi tunaweza sema kwamba hiki kitabu kina mamlaka ya kutuongoza sisi? Hakiwezi,” alisema.
“Ukristo ni kama ugonjwa, ni kutubebea akili, ni taasisi ambayo inalenga kuwapa nguvu watu wachache na kuwapokonya nguvu wengine wengi,” aliongeza.
Vivianne aidha alidokeza anasema hivyo kwa sababu aliwahi kuwa katika uhusiano wa mtu ambaye alikuwa anajiita mtumishi wa Mungu lakini akaja kuibuka kuwa mwiba mchungu kwenye komborera lake la mapenzi.
“Nimekuwa katika chuo cha masomo ya Biblia, ilikuwa vizuri. Nimekuwa katika uhusiano na mtu aliyejiita mtumishi wa Mungu, lakini kiwango cha uchungu, mateso na kudhibitiwa ambako kuko kule kunaweza kupeleka katika kifo chako. Kwa hivyo niamini wakati ninakuambia kwamba Ukristo ni itikadi mbaya,” alisisitiza.