In Summary

•Bahati alikiri kujikuta akitoa machozi hadharani kwa kushindwa kuelewa ni kwa nini alitakiwa kujiondoa baada ya kukabidhiwa tiketi.

•Bahati alikiri kwamba wakati mwingine alipoonekana akilia hadharani katika kampeni, alikuwa akijifanya tu.

Kevin Bahati,akihutubia wanahabari siku ya JUmatatu Aprili/25/2022 katika hoteli ya Luke Nairobi
Image: WILFRED NYANGARESI

Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefunguka kuhusu masaibu yake katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Mwaka jana, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliwania kiti cha ubunge cha Mathare kwa tikiti ya Jubilee na mara kadhaa wakati wa kipindi cha kampeni alirekodiwa akilia hadharani. Katika wakati mmoja mahususi, alionekana akilia baada ya kuombwa ajiondoe kwenye kinyang’anyiro kwa ajili ya mwaniaji wa ODM Antony Olouch.

Wakati akizungumza na mchekeshaji Chipukeezy kwenye kipindi cha Chipukeezy Show, alikiri kujikuta akitoa machozi hadharani kwa kushindwa kuelewa ni kwa nini alitakiwa kujiondoa baada ya kukabidhiwa tiketi wakati akiwa na uhakika kabisa kuwa angewashinda wapinzani wake.

“Machozi ilikuwa inatoka juu siamini nishapewa tiketi na naambiwa nistep down na huniambii sababu, sielewi ni kwa nini. Naona kabisa huyu jamaa namshinda, kabisa!” Bahati alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 hata hivyo alikiri kwamba wakati mwingine alipoonekana akilia hadharani katika kampeni, alikuwa akijifanya tu.

“.. lakini kuna saa pia nilikuwa naamua leo nitalia. Kipindi,” alisema.

Bahati wakati uo huo alidai kuwa licha ya kuwania kwa tikiti ya Jubilee, alikuwa kama mgombeaji huru kwani chama cha Jubilee kilichoongozwa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta hakikuwahi kumpa uungwaji mkono wowote.

Alifichua kuwa alitumia takriban Ksh 27milioni kutoka kwa mifuko yake mwenyewe.

“Nilikuwa tu niko Jubilee lakini nilikuwa mgombea huru. Kwa sababu sasa, hata na tiketi hii Jubilee siungwi mkono. Nilipelekwa tu IEBC tiketi juu nishapewa hakuna chaguo lingine, hiyo haingerudishwa nyuma. Njia pekee ilikuwa niirudishe na mimi niseme nimeacha kusimama,” Bahati alisema.

Aliongeza, “Lakini ilikuwa kila kitu niko independent. Nilifanya kampeni na pesa zangu mwenyewe hadi mwisho. Ni takriban shilingi milioni 27.

Bahati alikiri kuwa kuwania kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee ni mojawapo ya makosa makubwa aliyowahi kufanya maishani mwake akisema kuwa ikiwa angewania kiti hicho kwa tikiti ya UDA sasa angekuwa Bungeni.

“Kama ningekuwa na tikiti hiyo, ningekuwa bunge. Hilo lilikuwa mojawapo ya makosa makubwa niliyowahi kufanya katika maisha yangu, kuikimbia UDA wakati huo,” alisema.

Hata hivyo aliongeza, "Sijutii chochote. Sifanyi hivyo kwa sababu ufunguo wa mafanikio ni kuanzia wakati hauko tayari.”

Bahati aliwania kiti cha Ubunge wa Mathare katika uchaguzi wa Agosti 2022 na aliibuka nambari tatu nyuma ya Anthony Oluoch wa ODM na Billian Ojiwa wa UDA.

View Comments