In Summary

•Wahu alimkumbusha marehemu kuhusu mapenzi mazito ambayo bado anayo kwake na jinsi anavyomkumbuka.

•Mke huyo wa mwimbaji Nameless alifichua kwamba habari za kifo cha baba yake miaka kumi iliyopita zilimvunja moyo sana.

Wahu Kagwi na marehemu baba yake GS Kagwi
Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Siku ya Jumatano, mwanamuziki mkongwe wa Kenya Wahu Kagwi aliadhimisha mwongo mmoja tangu baba yake mpendwa kufariki.

Huku akimkumbuka mzazi huyo wake kupitia Facebook, Wahu alisema kwamba ilikuwa baraka kubwa sana marehemu kuwa baba yake.

Alichukua fursa hiyo kumkumbusha marehemu kuhusu mapenzi mazito ambayo bado anayo kwake na jinsi anavyomkumbuka.

"Siwezi kuamini kuwa tayari ni miaka 10 tangu uende kuwa na Bwana. Bado nakumiss sana, hasa siku kama za leo 💔. Ulikuwa baba mzuri sana. Baba aliye mbele ya wakati. Mume ambaye alimfanya mama ajisikie salama na maalum," Wahu aliandika kwenye Facebook siku ya Jumatano, Januari 11.

Babake Wahu, Bw GS Kagwi alifariki dunia mnamo Januari 11, 2013. 

Wahu amesema kwamba marehemu alikuwa rafiki wake wa dhati na kielelezo kwa vijana wengi sana kabla ya kifo chake.

"Ungefurahi sana kukutana na Shiru, nikijua jinsi ulivyopenda watoto. Lakini najua unatabasamu kwa lile tabasamu lako zuri 🙂😊," alisema.

Mke huyo wa mwimbaji Nameless alifichua kwamba habari za kifo cha baba yake miaka kumi iliyopita zilimvunja moyo sana.

Alisema alilia kila siku kwa miezi mitatu iliyofuata hadi wakati marehemu babakee alipomtokea katika ndoto na kumwambia imetosha.

"Kweli, karipio hilo lilifanya kazi 😂. Hatimaye niliweza kuamka kitandani na kurudi kwenye "maisha". Miaka 10 imepita, tunakukumbuka na tunakumiss. Utakuwa milele katika mioyo yetu. Endelea kupumzika kwa amani baba. Ninakupenda, nakupenda, nakupenda," alisema.

Takriban miezi miwili iliyopita, Wahu alifunguka jinsi baba yake alivyokuwepo siku zote kwa ajili yake na ndugu zake walipokuwa wakikua.

Alifichua kuwa Bw Kagwi angeacha kazi yake ili tu kumtazama tu akishiriki katika hafla za shule kama vile michezo, tamasha za muziki na mijadala. Pia wangeshiriki muda pamoja kila wakati ambapo babake hakuwa kazini.

"Sasa vile mimi ni mtu mzima najiuliza alikuwa anamwambia nini bosi wake wakati tulipotoka kazini bila mpangilio kuja kunitazama nasoma shairi au kitu kingine," alisema.

Mama huyo wa binti watatu alifichua kuwa yeye na babake walikuwa na uhusiano wa karibu sana na walikuwa wazi kwa kila mmoja kiasi cha kwamba walizungumza kuhusu karibu  kila kitu kilichokuwa kikiendelea maishani mwake.

"Tulizungumza kuhusu chochote na kila kitu; kuanzia kwa wavulana niliowapenda, shida zangu na kutojiamini, siasa, ndoto zangu, chochote tu. Tukawa karibu sana, hata nilipotaka kwenda club kwa mara ya kwanza, sikuweza kusema uongo, nilikuwa wazi naye. Ni wazi alikuwa na hofu juu ya hilo, lakini nilimwambia aamini jinsi alivyonilea. Aliniruhusu niende, lakini akamwambia kaka yangu mkubwa anisindikize," Wahu alisema.

Wahu pia alifichua kwamba babake pia alimsaidia kuhama na kukaa alipokuwa akianza maisha ya peke yake.

Pia alieleza jinsi mzazi huyo wake alimsaidia kupambana na masuala ya kisaikolojia alipokuwa kijana.

"Katika wakati wa giza tele maishani mwangu (nikiwa kijana) nilipopatwa na msongo wa mawazo(hadithi ya siku nyingine) kulikuwa na wakati kitu pekee ambacho kilinizuia kujitoa uhai ni jinsi baba yangu angenipeza, na kujilaumu mwenyewe 💔 💔"

View Comments