In Summary

•Rafiki wa mwanawe Nonini alizaliwa mvulana lakini hatimaye alibadilika na kuwa msichana baada ya kuzungumza na wazazi wake kuhusu hilo.

•Nonini alibainisha kuwa taratibu zote za kubadilisha rafiki wa mtoto wake kuwa msichana tayari zimefanyika na sasa anajitambulisha kama msichana.

Rapa Nonini na mwanawe
Image: INSTAGRAM// NONINI

 Mwanamuziki mkongwe wa Kenya Hubert Mbuku Nakitare almaarufu Nonini amezungumza kuhusu maisha ya Marekani na kuangazia baadhi ya tofauti za kipekee za nchi hiyo na Kenya.

Wakati akishiriki mazungumzo na Mwafreeka kwenye podcast ya Iko Nini, rapa huyo ambaye alihamia USA mwaka wa 2021 alibainisha kuwa maisha katika nchi hiyo ya magharibi ni tofauti ya kushangaza sana.

Alifunguka kuhusu moja ya mambo ya kushangaza zaidi aliyoshuhudia huku akifichua kuwa rafiki mkubwa wa mwanawe shuleni ni mtoto ambaye alibadilisha jinsia yake.

“Amerika ni noma. Kama mtoto wangu, rafiki yake wa karibu shuleni sasa ni kijana-msichana. Sijui kama ninaeleweka, huyo ni rafiki yake bora,” Nonini alisema.

Alifichua kwamba rafiki wa mwanawe alizaliwa akiwa mvulana lakini hatimaye alibadilika na kuwa msichana baada ya kuzungumza na wazazi wake kuhusu hilo.

“Mimi nilimuuliza “huyu ni dame ama ni chali?” ananiambia ni chali alafu aligeuka dame. Namuuliza kamaniambia yeye mwenyewe alijigeuza, akaniambia (rafikiye) aliambia wazazi wake anataka kuwa msichana,” alisema.

Rapa huyo alibainisha kuwa taratibu zote za kubadilisha rafiki wa mtoto wake kuwa msichana tayari zimefanyika na sasa anajitambulisha kama msichana.

“Jina lake huwa ni la mvulana. Mimi humuuliza (mwanawe) mbona anaitwa hivyo. Ananiambia ni mvulana lakini aligeuka kuwa msichana,” alisema.

Nonini alisema kuwa mtoto wake pia alimthibitishia kuwa rafiki huyo ambaye yuko naye darasa la 6 ndiye aliyefanya uamuzi wa kubadili jinsia yake.

Mwanamuziki huyo alizungumza kuhusu hayo alipokuwa akizungumzia hitaji la mzazi kuwa katika maisha ya watoto wao, haswa huko Marekani ambapo mtoto anakutana na watu wengi wenye njia tofauti za maisha.

View Comments