In Summary

•"Pole, nimekuwa nakumezea sana nimeshindwa kuzificha hisia zangu," ujumbe wa mwanadada huyo  kwa Ringtone ulisoma.

•Apoko ambaye amekuwa mseja kwa muda mrefu alimtaka mwanadada huyo kumtafuta Yesu badala ya yeye.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwenyekiti wa Muungano wa Wasanii wa Nyimbo za Injili nchini Kenya wa kujitangaza, Ringtone Apoko ameonyesha screenshot ya mazungumzo yake ya WhasApp na mwanamke aliyefungua roho ya kumimina moyo wake kwake.

Picha ya skrini ambayo mwimbaji huyomkongwe wa nyimbo za injili alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Alhamisi asubuhi ilionyesha mwanadada asiyetambulishwa akikiri mapenzi yake makubwa kwake.

"Pole, nimekuwa nakumezea sana nimeshindwa kuzificha hisia zangu," ujumbe wa mwanadada huyo  kwa Ringtone ulisoma.

Huku akimjibu, Apoko ambaye amekuwa mseja kwa muda mrefu alimtaka mwanadada huyo kumtafuta Yesu badala ya yeye.

'Okoka tu Yesu anakupenda," alijibu.

Mwanadada huyo hata hivyo alimhakikishia Ringtone kwamba tayari ameokoka, jambo ambalo mwimbaji huyo alitilia shaka.

"Umeokoka na unamezea kondoo mate?" Ringtone alihoji.

Mwanamke huyo ambaye alionekana kutokuwa tayari kuchukua 'HAPANA' kama jibu alihoji jibu la mwanamuziki huyo aliyezingirwa na utata mwingi huku akiuliza ni uhalifu gani alioufanya kwa kukiri hisia zake.

"Kwani kukupenda ndio uniambie niokoke? Kwa hivyo kupenda ni vibaya? Wewe sasa ni kondoo?" alimuuliza Ringtone.

Ringtone amekuwa single kwa muda mrefu na mara kadhaa amejitokeza kuwaomba wanawake wanaomcha Mungu kuomba nafasi ya kuwa mke wake. Amewahi kubainisha kwamba anataka mke anayejua kuomba.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, mwimbaji huyo alidai kwamba hatimaye amefanikiwa kupata kipenzi cha maisha yake.

Katika klipu aliyopakia, mwanamuziki huyo aliyezingirwa na utata mwingi alidai kuwa amezama ndani kabisa kwenye mahaba.

"Nafurahi sana. Mazee nimezama kwenye mahaba. Nashukuru Mungu kwa kunisaidia kuzama kwenye mapenzi," alisema.

Mwenyekiti huyo wa kujitangaza wa Muungano wa Wasanii wa Injili wa Kenya alibainisha kuwa mapenzi yake mapya ni matamu sana.

Alisema kuwa anafurahi sana kwa mahusiano yake mapya na kubainisha kuwa hakuwahi kufikiria kwamba atapata mapenzi.

"Hivi karibuni nitawatambulisha kwa mpenzi wangu. Nimeanguka katika mapenzi mazee," alisema.

Aidha aliwashukuru mashabiki wake kwa kumuombea hadi akafanikiwa kupata mpenzi na kujikita katika mahusiano.

View Comments