In Summary

•Vishy amefichua kuwa dada yake ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 9 alizaliwa akiwa na hali ya tawahudi.(Autism)

•Vishy alifichua kwamba mama yake angelia takriban kila siku kutokana na hali ya binti huyo wake mdogo.

• Ameeleza kuwa hali ya dadake hufanya awe na nguvu zaidi ikiwa tahadhari za daktari hazifuatwi.

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy
Image: SAIDI ABDALLA

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy amesema anatia bidii zaidi kazini ili aweze kumtunza dadake mdogo ambaye amekuwa akiishi na ulemavu.

Vishy amefichua kuwa dada yake ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 9 alizaliwa akiwa na hali ya tawahudi.(Autism)

"Dadangu hakulia alipozaliwa. Shingo yake ilikuwa imeinama. Mama yangu alidhani ni kawaida tu. Hata alipokuwa akikua ilikuwa nadra sana kwa dadangu kulia. Hata akihisi njaa hakuwa akilia, dadangu alikaa hapo tu kama mchongo," Vishy alisimulia akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Alisema iliwachukua takriban miaka miwili baada ya dada yake kuzaliwa kutambua kwamba hakuwa kawaida.

Vishy alifichua kuwa wakati dadake alikuwa akitambaa angeweza kuchua viumbe watambaao na kuanza kuwala.

"Mama yangu alisema ni lazima afanye jambo. Dadangu alipelekwa hospitali akapimwa ikasemekana hayupo sawa." Alisema.

"Usiku dadangu angeamka wakati sote tumelala hatusikii alafu anaenda anachukua  unga ya ugali, ya ngano, omo anazichanganya kisha anaanza kujipaka. Tuliwahi kuamka asubuhi tukapata amejipaka gundi," 

Baada ya hali ya dadake Vishy kugundulika, alianza matibabu. Vishy ameeleza kuwa hali ya dadake hufanya awe na nguvu zaidi ikiwa tahadhari za daktari hazifuatwi.

"Ako na autism.Hafai kula sukari au maziwa kwa sababu akila anakuwa nguvu zaidi,"

Vishy alifichua kwamba mama yake angelia takriban kila siku kutokana na hali ya binti huyo wake mdogo.

Alisema kwa sasa hali ya dadake sio nzuri licha ya juhudi nyingi walizofanya, jambo ambalo linamuathiri kisaikolojia pamoja na mama yake.

"Nataka kufikia wakati namleta Nairobi niwe imara kifedha na ninunue vitu vya nyumba. Nataka angalau ninunue samani. Nataka awe starehe. Nataka dadangu aishi maisha ya kawaida kama watoto wengine," Alisema.

Vishy ameanzisha biashara mtandaoni ili aweze kupata fedha za kufadhili malezi ya dada huyo wake.

Pia ametoa ombi kwa wasamaria wema ambao wangependa kumsaidia dadake kumfikia kwa njia ya simu au mitandao ya kijamii.

View Comments