In Summary

•Jay alisema kwamba alikuwa katika hali mbaya sana akibainisha kwamba Mungu alimuokoa kutokana na hali hiyo.

•Jay aliwashukuru wahudumu wa afya ambao walifanya juu chini kuhakikisha kuwa afya yake imerejea hasa alipokuwa ICU siku 127.

Profesa Jay
Image: HISANI

Mwanamuziki nguli wa Bongo Hiphop Joseph Haule almaarufu Profesa Jay hatimaye amevunja kimya kwenye mitandao ya kijamii miezi kadhaa baada ya kupambana na ugonjwa hatari ambao ulitishia maisha yake.

Katika chapisho lake la kwanza baada ya takriban mwaka mmoja na miezi minne, ambaye pia ni mbunge wa zamani wa eneo la Mikumi nchini Tanzania alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya afya yake baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini ambapo alibainisha kuwa sasa yupo imara na anaendelea vizuri.

Jay alisema kwamba alikuwa katika hali mbaya sana akibainisha kwamba Mungu alimuokoa kutokana na hali hiyo.

"Kwanza namshukuru sana MUNGU aliye hai kwa uponyaji na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuwa hai, Hali yangu ilikuwa mbaya isioelezeka, Asante sana Mungu baba, nitakutukuza na kukusifu siku zote za maisha yangu," alisema katika taarifa ambayo alichapisha kwenye mtandao wa Instagram.

Mwanamuziki huyo mkongwe aliendelea kutoa shukrani za dhati kwa wote ambao walisimama naye katika kipindi cha maumivu yake wakiwemo rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye aligharamia matibabu yake, kiongozi wa chama cha CHADEMA Freeman Mbowe miongoni mwa viongozi wengine.

"Namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dr. Samia Hassan Suluhu na Serikali yake kwa kunigharamia matibabu yangu yote ya Muhimbili na Nje ya Nchi ,Asante sana Mama pamoja na serikali yako yote kwani viongozi wako wa chama na serikali walikuwa wanapishana kila siku kuja kuniona na kunifariji."

Namshukuru sana Mwenyekiti wa chama changu cha CHADEMA Kamanda @freemanmbowe ,Wanachama na viongozi wote waandamizi wa chama kwa jitihada zao za kuhakikisha napata matibabu bora zaidi kwa kushirikiana na serikali." alisema.

Jay pia aliwashukuru wahudumu wa afya ambao walifanya juu chini kuhakikisha kuwa afya yake imerejea hasa alipokuwa ICU siku 127.

"Zaidi nawashukuru sana Madaktari na Manesi wote wa muhimbili na kote nilikopitia kwa kunipa matibabu ya kiwango cha juu kwa zaidi ya mwaka mzima niliolala hapo Muhimbili hasa zile siku 127 za hatari nilizokuwa nimelazwa ICU, mlijitoa kwa uwezo wenu wote kuhakikisha kuwa mnaokoa uhai wangu ,AHSANTENI SANA."

Kwa umuhimu mkubwa sana nawashukuru sana Watanzania wote mliojitolea kwa maombi na michango ya fedha zenu kuhakikisha natibiwa na kusema ukweli ilinisaidia sana kulipa bills za awali kabla ya serikali kuamua kuingilia kati na kuubeba mzigo huu asanteni sana na sitowasahau.

Isitoshe, alitoa shukrani za dhati kwa watumishi wa Mungu kwa kumuombea hadi kufikia hatua ya kupata afueni hatimaye.

Aidha, alishukuru familia yake yake kwa ushirikiano mkubwa na upendo walioonyesha wakati wa ugonjwa wake.

View Comments