In Summary

•Bi Rachel Ruto alikiri mapenzi yake kwa mumewe na kusimulia furaha yake kubwa na kuridhika kwake naye.

•Rachel na Ruto walifunga ndoa mwaka wa 1991 na kwa sasa wao ni walezi wa watoto saba.

Bi Rachel Ruto akimlisha keki rais William Ruto.
Image: X/MAMA RACHEL RUTO

Leo hii, Desemba 21, ni siku ya pekee sana kwa rais William Samoei Ruto na mkewe Rachel Ruto.

Rais wa tano wa Kenya anasherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 57 hivi leo na vile vile anaadhimisha miaka 32 ya ndoa yake.

Huku akimsherehekea mume wake katika siku yao maalum, Bi Rachel alikiri mapenzi yake kwake na kusimulia furaha na kuridhika kwake naye.

“Siku ya Kuzaliwa yenye Furaha, Bill, rafiki yangu mpendwa na msiri wangu. Katika siku hii muhimu, tunapoadhimisha siku yako ya kuzaliwa na maadhimisho ya harusi yetu, ninajawa na shukrani,” Bi Rachel Ruto alisema kupitia Twitter.

Aliongeza, “Nikitafakari juu ya safari ambayo tumeshiriki, nakumbushwa mstari wa Biblia, “Kuna mambo matatu yatakayodumu—imani, tumaini, na upendo—na lililo kuu zaidi kati ya hayo ni upendo.” 1 Wakorintho 13:13. Kwa kweli mambo ni matatu  . Upendo wako na msaada umekuwa baraka ya kweli. Asante kwa kuwa chanzo cha daima cha furaha na nguvu.”

Mke wa rais wa Kenya aliambatanisha ujumbe wake mzuri na picha akimlisha rais keki.

Wawili hao walioingia ikuluni Agosti mwaka jana pia wanasherehekea kumbukumbu ya ndoa yao leo. Walifunga ndoa rasmi mnamo Desemba 21, 1991 na wamekuwa pamoja kwa miongo mitatu iliyopita.

Wakati akikumbukuka safari ya ndoa yao, Ruto, katika mahojiano ya awali, takriban mwongo mmoja uliopita, alisema alikutana na kipenzi cha maisha yake katika kanisa ambalo wote walihudhuria.

"Alikuwa mshiriki wa kwaya kama mimi, sote tulikuwa washiriki wa timu ya Uinjilisti inayoitwa timu ya uinjilisti ya North Rift," alisema.

Ruto alisema alikuwa mwinjilisti wakati huo.

"Tulikuwa tukienda misheni pamoja sehemu mbalimbali. Alifanya kozi ya elimu," alisema.

Rachael, baada ya elimu yake ya sekondari katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere, alisomea Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

"Alitumwa katika shule ya wasichana ya Kessup kwa mazoezi ya kufundisha na mimi kwa ujumla nilikuwa karibu na ndipo historia yetu ya mapenzi ilipokua. Mengine ni historia," Ruto alisema.

Rachel na Ruto walifunga ndoa mwaka wa 1991 na kwa sasa wao ni walezi wa watoto saba.

View Comments